SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumamosi, 9 Septemba 2017

T media news

Breaking: Serikali yataifisha Alamsi ya Mgodi wa Mwadui

Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt Philip Mpango amemuagiza Kamishna wa Madini Tanzania kutaifisha madini ya Almasi yaliyokamatwa katika Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.

Madini hayo yalizuiwa dakika 5 kabla ya ndege iliyokuwa ikitakiwa kuyasafirisha kwenda nchini Ubelgiji kuanza safari ambapo maafisa wa serikali katika uwanja wa ndege walisema kwamba yalitakiwa kupimwa upya baada ya kuyatilia mashaka.

Akizungumza wakati wa ukaguzi wa madini hayo, Kamishna wa Madini alisema kuwa, mgodi unapokutwa na kosa la kufanya uthaminishaji wa madini usio sahihi, adhabu zinazoweza kuchukuliwa dhidi yake ni pamoja na kufutiwa leseni ya biashara au madini yake kutaifishwa na serikali.

Awali madini hayo yalipokamatwa ilielezwa kuwa yana thamani ya USD 14 milioni (Tsh 31.4 bilioni) lakini baada ya kupimwa na watalaamu katika uwanja wa ndege ilibainika kuwa yana thamani ya USD 29 milioni (Tsh 64 bilioni).

Kabla ya kuingia katika chumba kilichokuwa kimehifadhia madini hayo, Waziri Philip Mpango alitoa maagizo kwa vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na taasisi nyingine za serikali ikiwamo TAKUKURU, TRA, BoT na Ofisi ya Kamishna wa Madini kushirikiana kwa pamoja kikamilifu kuhakikisha kuwa rasilimali za watanzania haziibiwi.

Kuhakikisha anadhibiti mianya ya wizi wa madini, Waziri Mpango ameagiza upimaji ufanyike katika mgodi wa madini na uwanja wa ndege ili kujiridhisha na kiwango cha madini yanayotolewa.

Aidha, Waziri Mpango ameagiza wawakilishi wote aliohusika kuthaminisha madini ya Almasi katika Mgodi wa Mwadui wachukuliwe hatua za kisheria kutokana na kuthaminisha madini kwa kiwango cha chini na hivyo kusababisha serikali kupoteza mapato.

Akitoa maagizo kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Mwadui, Prof. Mruma, Waziri Mpango amemtaka awafikishie ujumbe wenzake kwamba mwaka huu serikali inataka gawio na haitaki makombo kwani imechoka kusubiri.

Wakati huo huo, Waliokuwa Mawaziri wa Nishati na Madini kwa vipindi tofauti, Prof. Sospeter Muhongo, na  William Ngeleja wametakiwa kufika katika ofisi za Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), ili kuhojiwa kutokana na kutajwa katika ripoti za uchunguzi wa biashara ya madini ya Tanzanite na Almasi.