Kuelekea mchezo wa Ngao ya Jamii kwa ajili ya kuzindua msimu mpya wa ligi ku Tanzania bara mnyama Simba na mabingwa wa Tanzania Yanga wote wamekimbilia Zanzibar kwa ajili ya kujiandaa na mchezo huo.
Yanga wameondoka Unguja asubuhi ya August 14 kuelekea Pemba wakati Simba wao wakiwasili jioni ya siku hiyohiyo wakitokea Dar. Imekuwa kama tamaduni kwa vilabu hivi pindi inapokaribia mechi yao wanalikimbia jiji la Dar es Salaam na mara nyingi wamekuwa wakielekea Zanzibar kwa ajili ya kuweka kambi ya maandalizi.
Yanga wamekuwa wanakimbilia Pemba wakati Simba hukaa Unguja. Unguja na Pemba ni visiwa viwili ambavyo vyote vipo ndani ya Zanzibar. Yanga walipita Unguja kama njia tu ambapo waliwasili August 13 na usiku wake wakacheza mechi ya kirafiki dhidi ya Mlandege na kupata ushindi wa magoli 2-0 wafungaji wakiwa ni Ibrahim Ajib na Emanuel Martin.
Jana asubuhi wakaelekea zao kisiwani Permba kuweka kambi ya maandalizi kwa ajili ya mechi yao ya Ngao ya Hisani mchezo utakaopigwa Augst 23, 2017.
“Sisi hapa ni myumbani mara zote tunapopata nafasi ya kujiandaa na mechi yoyote iwe kubwa au ndogo tunapenda kuja Zanzibar kwa sababu mazingira ni rafiki kila kitu kwetu hapa kinakuwa sawa. Tunamchezo na watani zetu wa jadi Yanga tumeona tuje tukae Zanzibar hadi tarehe 22 ndio turudi zetu Dar kwa ajili ya kucheza mechi hiyo,” Abbas Selemani mratibu wa timu.
Simba ina kikosi cha wachezaji 23, leo ataongezeka mchezaji mmoja wa mwisho Juuko Murshidi ambaye tayari ameshawasili Dar lakini Erasto Nyoni amesafiri kwenda Burudi kwenye msiba wa baba mkwe wake.