Watu watatu wakiwamo watoto wadogo wawili wamekufa huku wawili wakinusurika baada ya mtumbwi waliokuwa wakisafiria kuzama kwenye mto Ruvu, walipokuwa wakijaribu kuvuka kutoka Vigwaza kwenda Mlandizi mkoani Pwani.
Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Jonathan Shana alisema licha ya watu hao kubainika kufa, nahodha wa mtumbwi huo hajulikani alipo. Shana alisema ajali hiyo imetokea Jumamosi saa 4:00 asubuhi kwenye mto Ruvu wilaya ya kipolisi Chalinze.
“Ajali hiyo imepoteza maisha ya watoto wawili ambao ni Nusrat Haji miezi minne na Feisal Hamza mwenye umri wa mwaka mmoja na nusu pamoja na Sikuzani Musa (41), ambaye mwili wake bado haujapatikana,” alisema Kamanda Shana.
Kamanda Shana aliwataja walionusurika ni Zuwena Ramadhan (29) na Tero Mziray (20) ambapo dereva wa mtumbwi huo hajulikani alipo na inaaminika hakufa maji.
“Chanzo cha mtumbwi huo kuzama bado kinachunguzwa na miili ya marehemu imefanyiwa uchunguzi na kukabidhiwa ndugu zao kwa ajili ya mazishi,”aliongeza.
Aliwataka wamiliki wa vyombo hivyo kuhakikisha vinakuwa kwenye hali nzuri ili kuepukana na ajali kama hizo ambazo zinapoteza uhai wa watu kutokana na ubovu.