Ulaji wa nyama una faida lukuki kwa afya ya binadamu ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa virutubisho vya aina ya protini ambayo ni rahisi kutumika mwilini, madini mbalimbali (Calcium, Magnesium, Phosphorus, Zinc na Chuma); vitamini aina ya folic asidi, E, B na B12 ambayo inapatikana katika nyama pekee.
Nyama pia inasaidia katika ukuaji na kuongeza afya ya mlaji kutokana na uwezo mkubwa wa kujenga mwili, kukarabati seli za mwili zilizokufa, kuzalisha chembe hai mpya, kurekebisha kinga ya mwili, kuongeza damu na kuimarisha mifupa.
Hata hivyo faida zote hizo zinapatikana tu, kwa walaji wa nyama iliyo bora na yenye kiwango. Hivyo ni vizuri wananchi wakazingatia kanuni za ulaji wa nyama yenye kiwango ili kujiepusha na athari zinazoletwa na nyama isiyo na kiwango.
Msajili wa Bodi ya Nyama Tanzania (TMB) Bi.Suzana Kiango amesema kuwa nyama yenye kiwango na bora huanzia kwenye utunzwaji wa mifugo wenye kuzingatia kanuni za uzalishaji bora, unenepeshaji wa mifugo yenye umri mdogo kwa kuwalisha chakula mchanganyiko kwa muda usiopungua siku 90 kabla ya kuchinja.
Bi.Kiango amesema kuwa hatua nyingine ni katika uchinjaji ambapo inashauriwa ufanyike kwenye machinjio bora ambayo yanakidhi viwango vya usafi. Hii ni pamoja na kuwa na sakafu na kuta zinazosafishika, maji ya kutosha na sehemu za kuning’iniza wakati wa kuchuna na kupasua.
“Kanuni za uchinjaji ni pamoja na kupumzisha mifugo ili kuipoteza fahamu na kumfanya mnyama asiogope na kuzalisha asidi nyingi inayosababisha nyama kuwa ngumu, pia iwe rahisi kutoa damu yote katika misuli. Uning’inizwaji wa chune mara baada ya kuchinjwa unasaidia kuondoa damu iliyo mwilini. Endapo damu haitatoka yote kwenye chune itasababisha nyama kuwa na rangi nyeusi na kuharibika mapema”, alisema Bi.Kiango.
Madhara ya ulaji wa nyama isiyo na viwango na bora ni pamoja na kupata magonjwa ya tumbo, kuharisha na kutapika endapo nyama itapata vimelea vya magonjwa hayo, kuugua magonjwa ya kuvimba miguu, kifua kikuu, shinikizo la damu, kisukari na kansa.
Hata hivyo, Bi. Kiango amesisitiza kuwa magonjwa haya yanaweza kuwatokea pia watu ambao hawatumii kabisa nyama kwa hivyo si nyama pekee ndio chanzo cha magonjwa haya japo inaweza kuwa sababu ya mtu kuugua.
“Bodi imeendelea kutoa elimu kwa watumiaji na wachinjaji wa nyama kupitia vyombo mbalimbali vya habari kama vile, redio, televisheni na magazeti. Pia katika maonesho mbalimbali kama Saba saba na Nane nane ambapo wataalamu wa bodi hutoa elimu kwa wananchi wanaotembelea mabanda ikiwa ni pamoja na kusambaza vipeperushi” amesema Bi.Kiango.
Namna nyingine ya kutoa elimu ni pamoja na kutumia matamasha ya nyama choma, wiki ya mayai na maonesho ya kuku, wiki ya chakula salama na siku ya chakula duniani. Wakati wa shughuli hizi wanashiriki hupatiwa elimu kuhusu faida na athari za kula nyama isiyo na viwango ili kunusuru afya zao.
Aidha walaji huelekezwa maeneo mbalimbali wanayoweza kupata nyama hiyo, na kwa upande wa wafanyabiashara wa nyama hupewa maelekezo ya kuboresha miundombinu ya kuzalisha, kuchinja na kuuza kwa kuzingatia viwango vya ubora na usalama.
Kutokana na baadhi ya wafanyabiashara ya nyama kuendelea kuwauzia walaji nyama isiyo na viwango kwa kujua au kutojua madhara ya nyama hizo, Bi.Kiango alisema kuwa Bodi inachukua hatua za kuhakikisha wafanyabiashara hao wanapata uelewa wa kutosha.
“Bodi imeanza kutoa mafunzo kwa watumishi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa ambao watashiriki katika kutekeleza majukumu ya Bodi ikiwa ni pamoja na kusimamia uzalishaji wa nyama na kuelimisha wachinjaji ,walaji na wadau wengine wanaojishughulisha na uzalishaji wa nyama”alifafanua Bi.Kiango.
Aliendelea kusema mafunzo hayo yameshatolewa kwa vitendo kwa watumishi wanne kutoka katika kila Mamlaka za Serikali za Mitaa za mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Morogoro na Dodoma ambapo hadi sasa jumla ya wadau 490 katika maeneo tajwa wamekwisha patiwa elimu hiyo. Pia mafunzo yanatolewa na wadau wengine ambao ni Chuo cha nyama cha VETA, Dodoma na Kampuni ya nyama ya jijini Arusha.