Na Salym Juma, Arusha
Kiungo mwenye heshima zake AC Milan na Juventus, Andrea Pirlo amewahi kukaririwa akisema kuwa Antonio Conte anapenda kuwa Bosi. Inawezekana watu wengi hawakuelewa kauli hii na kila mtu aliitafsiri kadiri alivyoweza. Kwa maana nyepesi ni kwamba Pirlo alimaanisha Conte huwa hapendi mchezaji fulani kujiona yeye ni bora kuliko wengine. Diego Costa alijikuta anaangukia upande wa pili wa Conte na kujifanya yeye ndie bosi. Costa alifika mbali zaidi na kutaka kumkalia Conte kichwani eti kisa yeye ndiye anaetegemewa baada ya Hazard.
Kutokana na suala hili Conte aliamua kumuandikia ujumbe mfupi wa maandishi Diego na kumtakia kila la heri katika timu atakayokwenda kwani hayumo kwenye mipango yake. Costa anatamani kurudi Atletco ambayo imefungiwa kusajili kwani hawezi kwenda tena nchini China kama alivyokuwa anataka. Leo tujaribu kuchimba sababu ambazo zinamfanya Conte kutomuhitaji kwenye mipango yake licha ya Diego kumpa taji katika msimu wake wa kwanza EPL. Inawezekana kuna vingi ila vichache vinaweza kuwa hivi hapa chini.
Katika mechi iliyochezwa 15 Oct 2016 kati ya Chelsea na Leicester City Diego Costa alionekana kumkaripia kocha wake Antonio Conte akimtaka amfanyie ‘sub’ akihofia kupata kadi ya pili ya manjano hasa baada ya kuwachezea faulu mara kadhaa wachezaji wa Leicester. Costa licha ya kufunga goli la uongozi katika mechi hii alionekana kukaba kwa hasira licha ya timu yake kuongoza magoli mawili hadi wakati huo kabla ya Moses kuhitimisha kwa kufunga goli la tatu. Kitendo hicho hakikumfurahisha Conte hata kidogo japo ‘alinywea’ ila kinyongo hakikumtoka na matokeo yake tunayaona sasa.
Conte ndiye meneja wa timu na yeye anayo mamlaka ya nani aanze nani asubiri. Kitendo cha Costa kumpangia meneja wake kwa kujifanya kaona umuhimu wa mechi dhidi ya United kiliwachukiza wapenzi wengi wa soka kutokana na ukweli kuwa nidhamu ni suala la msingi sana katika mpira. Lugha ya picha aliyoonesha Costa katika mechi hii haikumfanya Conte ampumzishe Costa na badala yake alimuacha hadi mwisho wa mechi, hicho ndicho kiburi cha ‘Dikteta’ Conte cha kutotaka kukawaliwa na mchezaji.
14 Jan 2017 Conte alisafiri takribani kilometa 143 na washambuliaji watatu watakaoanza, Willian, Hazard na Pedro huku jina la Costa likibaki London. Sababu kubwa ya Costa kuachwa ilielezwa na Conte kuwa ni majeraha yaliyokuwa yanamkabili mshambuliaji huyu kitu ambacho kilikinzana na magazeti ya London. Sababu za kuaminika ni kwamba Conte aligombana na Costa mazoezini hadi kufikia hatua ya Costa ‘kumkusanya’ Conte shingoni. Ili kuboresha morali ya timu na kuepusha migogoro kwenye mapambano, Mtaliano huyu aliamua kulifunika suala hili na kumtetea Costa kwa kigezo cha majeruhi.
Katika kipindi hicho Conte aliangalia morali ya wachezaji wake na shabaha yake kwa msimu hivyo hakupenda kuzungumza suala hili kwenye vyombo vya habari. Conte alijifunza kwa yaliyomtokea mtangulizi wake (Mourinho) ndio maana ilikuwa rahisi kumvumilia Costa ili amalize salama hasa ukiangalia hadi wakati huu Costa ndiye aliyekuwa ameonekana kuibeba timu hadi kuongoza ligi. Uongozi wa klabu pia ulimsihi Costa kutoongea chochote juu ya jambo hili ‘Proffesional player’ anavyopaswa kuwa.
Tianjin Quanjian ni miongoni mwa timu ambazo zilitangaza dau la kumng’oa Costa pale London katika majira ya January. Chelsea chini ya Conte haikuwa na mkakati wowote wa kumuuza Costa kwa kipindi hiki baada ya kuwakosa Washambuliaji iliyokuwa inawahitaji katika dirisha dogo (Morata na Lukaku). Hali hii ilimchanganya Costa kwani aliahidiwa mshahara mnono na timu za China. Tangu kutangazwa kwa habari hizi mwezi January Diego hakuonekana kucheza vizuri kama alivyokuwa anacheza mwanzo kutokana na kuharibika kisaikolojia.
Matatizo makubwa ya Conte na Costa yalianzia hapa kwani Costa hakutaka kucheza kwa moyo wote kuhofia kupata majeraha ambayo yangehatarisha uhamisho wake wa kwenda China kwani alijipa matumaini ya kukamilisha uhamisho kwenye dirisha kubwa kumbe sheria za usajili na malipo ya mishahara kwa vilabu vya China zitakuja kubadilika ila hakuna aliyejua hili kabla. Conte aliamini Costa ni msaliti kwani alitaka aisaliti Chelsea katikati ya mapambano kisa pesa.
Mechi baina ya Manchester United na Chelsea ilikuwa mbaya sana kwa Conte hasa baada ya mchezaji wake wa kutegemewa, Eden Hazard kukabwa vilivyo na kiungo wa Man United, Ander Herera. Kuna wakati Hazard alikabwa na Herera na Eric Bail kwa wakati mmoja. Diego Costa alikuwa ni miongoni mwa watu waliolaumiwa sana kwenye mechi hii kwani alipaswa kuonesha uzoefu wake baada ya mabeki wa Man U muda mwingi kuwa bize na Hazard badala yake muda mwingi alionekana kujiangusha na kunyang’anywa mipira wakati timu ilikuwa inahitaji kusawazisha na kurudisha morali ya mechi.
Conte japokuwa alizidiwa kimbinu na Mou ila naamini ‘kimoyo moyo’ aliishia kumlaumu Costa kwani hakuna alichokuwa anakifanya zaidi ya ‘kui-cost’ timu. Uzembe huu ulimfanya Conte aanze kumpa muda wa kucheza Mich Batshuay kwani aliamini Costa anahitaji changamoto ili arudi kwenye mstari jambo lilifanikiwa kwa kiwango fulani kwani Batshuay ndiye aliyewapa Chelsea ubingwa dakika za mwisho kwenye mechi dhidi ya West Bromwich.
Sababu hizi ndizo zinamjia kichwani Conte kila akilala kwani miongoni mwa makocha wenye viburi na wakorofi katika dunia ya sasa huwezi kumuacha Antonio Conte. Conte anajiamini ana uwezo mkubwa hivyo jambo ambalo limedhihirika msimu uliopita hivyo Costa hawezi kuwa mkubwa kuliko yeye hata mara moja. Pesa aliyopewa inatosha kumnasa mshambuliaji wa kiwango cha Dunia kwa kipindi hiki na tayari yupo kwenye hatua nzuri ya kukamilisha hilo.