SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumanne, 4 Julai 2017

T media news

Minykano ya Kisiasa na vijembe ndani ya Bunge...

MJADALA wa kujadili miswada ya rasilimali za madini ulianza jana Bungeni, huku ukigubikwa na minykano ya Kisiasa na vijembe ndani ya Bunge.

Miongoni mwa vijembe hivyo ni Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema, kumwambia Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene, kuwa anataka kuhamishwa wizara.

Mbali na Lema pia, Mbunge wa Geita Vijijini (CCM) Joseph Kasheku maarufu kama ‘Musukuma’ alisema mgombea urais wa Chadema katika uchaguzi mkuu wa 2015 na kuungwa mkono na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa, alipatikana kwa hati ya dharura, hivyo wapinzani hawatakiwi kupinga kuletwa kwa miswada bungeni kwa hati ya dharura.

Wakichangia mjadala wa Muswada wa sheria ya Mamlaka ya nchi kuhusiana na umiliki wa Maliasili wa mwaka 2017 na Muswada wa sheria ya mapitio na majadiliano kuhusu masharti hasi katika mikataba ya maliasili za nchi kwa mwaka 2017, wabunge hao walirushiana vijembe kutokana na wengi wa chama tawala kuunga mkono kupelekwa kwa hati ya dharura huku wabunge wa upinzani wakipinga.

LEMA
Lema alisema Bunge linapotunga sheria ni wakati muhimu wa kuwa makini na kwamba miswada hiyo ilihitaji muda wa kutosha.

Alisema pande zote za bunge ushabiki katika utungaji wa sheria umekuwa ni muhimu na thabiti kuliko umuhimu wa sheria yenyewe.

“Bunge hili tulipopitisha Sheria ya Uhujumu Uchumi hapa zilipigwa kelele, leo sheria zile zinakula watu wa upande huu kuliko wa upande ule,” alisema.

Aliongeza: “Ripoti ya makinikia ulikuwa unamsikia Rais akilalamika kwamba uongozi uliopita pamoja na Bunge ulifanya makosa makubwa katika utungaji wa sheria za madini.”

 Alieleza kuwa kama wapo makini na kubadilisha sheria hizo kwa ajili ya utawala bora, ingekuwa ni vyema muswada wa kwanza kupelekwa kwa dharura ungekuwa ni wa kuondoa kinga ya viongozi wanapokuwa madarakani kwa kuwa wamefanya maamuzi ya kutozingatia haki.

Kufuatia kauli hiyo, Simbachawene alisimama kuomba utaratibu akisema kuwa Lema amekiuka Kanuni ya 80(4)-(6) ambayo inaweka utaratibu wa namna ya miswada inayoletwa kwa hati ya dharura na kwamba hakuna sababu ya kulaumu kwa kuwa pande zote zilikaa na kukubali muswada uletwe bungeni.

“Sheria tunayotunga leo tunaweza kurekebisha tena hata Bunge lijalo tukija jingine tutarekebisha ndio kazi ya Bunge,” alisema Simbachawene.

Akiendelea kuchangia, Lema alisema kuna wengine wanataka kuhamishwa wizara ndio maana kila akisimama wanasimama kwa sababu wanajua umuhimu wa hizo wizara.

“Kwenye fedha za IPTL wabunge hawa na Simbachawene huyu huyu alisema fedha sio za serikali, leo mmekamata watu wako gerezani, tunapojenga hoja mko, kimya wote sisi ni Watanzania,” alisema.

Alisema anataka kuamini kuwa Rais aliyepo ni mzalendo na anapenda watu.

“Najiuliza kwa mamlaka aliyopewa Rais siku akija mtu si mzalendo kama Magufuli, nataka kuamini hivyo akatokea hata upande huu hata Chadema kwa sababu hakuna malaika, akitokea rais asiye mwaminifu na mmempa mamlaka ya kusimamia rasilimali zote na mkaliwekea Bunge masharti nafuu, Taifa hili litauzwa,” alisema Lema.

Alisema sheria inayotungwa haimuangalii Rais aliyepo madarakani bali inatungwa sheria kwa kufikiria anaweza kutokea rais ambaye sio malaika.

 MUSUKUMA
Kwa upande wake, Musukuma alisema Lowassa, alipatikana kwa hati ya dharura kwa sababu walimuona anafaa kwa dharura aliyokuwa nayo.

Alisema Lowassa alikuwa hajui mambo yoyote ya Chadema, hakushindanishwa na mtu yeyote katika chama hicho, lakini alipewa dharura ya kugombea urais.

“Nawashangaa wabunge wanaolalamika kwamba wanaburuzwa katika kutunga sheria, lakini walileta mtu ambaye wanataka akabidhiwe nchi, na hajui chochote kuhusu Chadema,” alisema Musukuma.

Musukuma alisema mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambaye sasa ni Rais John Magufuli, alipatikana kwa kufuata utaratibu wa CCM.

“Wabunge wote wa CCM tunaunga mkono hati ya dharura ya serikali kwenye miswada hii kwa kuwa tumeibiwa vya kutosha. Nimesikia wanalalamika sana wanasema tumechelewa kufanya mabadiliko, mimi nakubali tumechelewa kwa sababu dunia inabadilika na CCM inabadilika,” alisema Musukuma.

Aliongeza: “Watu waliokuwa wanatuchelewesha wote mnawakumbatia nyie huko, serikali hii ilikuwa inaongozwa na Lowassa na Sumaye (Fredrick), ndio mmewakumbatia kwenu, sisi tulipoona hawafai nyinyi mmewachukua kwa hati ya dharura, kwa hiyo mtulie tumeamua kufanya mabadiliko kwa Majaliwa (Kassim) na mheshimiwa Magufuli.”

Aliongeza wapinzani wanalalamika kwamba serikali imefanya mabadiliko ya sheria haraka haraka na mwaka 1992 yalifanyika mabadiliko kwenye siasa na bila ya mabadiliko hayo, wapinzani wasingekuwapo kwani wote wangekuwa CCM.

  ZITTO
Naye, Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe, alisema kazi wanayofanya ni muhimu, lakini mijadala hailingani na uzito wa jambo lililopo.

“Tulijadli jambo hili kwa utulivu, kurushiana maneno kunatupotezea muda, kuna sheria tatu, sheria moja ni kubwa inayohusu mabadiliko ya sheria ya madini,” alisema Zitto.

Alisema sheria mbili zilizobaki ni mambo ambayo yalipaswa kufanyika tangu mwaka 1962, lakini hayakufanyika, hivyo kwa sasa wanafanya masahihisho ya makosa.

“Sheria hizi mbili za kimapinduzi kwa kuwa kwa mara ya kwanza tumekuwa nchi ya kwanza ya Kiafrika kutamka kwenye sheria kwamba chochote kilichopo juu na chini kwenye nchi yetu ni mali yetu.”

Aliongeza: “Lakini hatujabadili mfumo wa uzalishaji, mfumo ni ule ule, sheria iliyopita ina umiliki, sheria ya mwaka 1979 ilikuwa na umiliki, si jambo jipya, jambo jipya tubadilishe mfumo wa uwekezaji.”

Alisema mwekezaji awe mkandarasi. “Mfano akija Acacia unakubaliana naye achimbe kwa niaba yako, aondoe gharama zake kinachobakia mgawane. tunafanya hivyo katika gesi ndio maana hakuna malalamiko makubwa,” alisema Zitto.

  MNYIKA
Mbunge wa Kibamba (Chadema), John Mnyika, Alisema wabunge wametoka katika toba badala ya kutubu wanarudia katika makosa kwa kulitaja jina la Mungu.

“Wenzetu wa CCM hamna uhuru kwenye chama chenu na mnasababisha Bunge kukosa umoja, dhambi hizi za kulitaja jina la Mungu inaambatana na matumizi mabaya ya rasilimali zetu, badala ya kuleta sheria bora, mmeamua kutenda dhambi kwa kuleta miswada ijadiliwe kwa hati ya dharura, hii ni dhambi mbele ya Mwenyezi Mungu,” alisema Mnyika.

Alisema kabla ya kujadili miswada hiyo Bunge lingeletewa ripoti zote mbili za makinikia, zijadiliwe kisha liielekeze serikali ifanye nini ndipo miswada iletwe.

Kuhusu muswada, Mnyika alisema sheria imetoa mamlaka makubwa kwa Rais kuhusu umiliki wa rasilimali za nchi.

“Sheria imedhihirisha kwanini tulitaka rasimu ya Jaji Joseph Warioba kupunguza mamlaka ya Rais,” alisema Mnyika.
  DEO SANGA
Mbunge wa Makambako (CCM), Deo Sanga, alisema muswada huo ni mzuri kwa kuwa ni jambo jema ambalo limekuwa likizungumzwa sana kipindi cha nyuma, lakini sasa limeletwa kufanyiwa marekebisho.

Alisema sheria hiyo, itawapa wananchi fursa ya kunufaika moja kwa moja na ajira, bima na kwamba halmashauri zinazungumza mahitaji yao na uwekezaji.

Sanga alisema sheria hiyo itadhibiti maliasili zinazopatikana na pia wadau wengi wameunga mkono marekebisho hayo.

  RIZIKI NGWALI
Mbunge wa Viti Maalum (CUF), Riziki Ngwali, alisema alikuwa ni miongoni mwa wajumbe wa Tume ya Jaji Warioba ambayo ilipokea maoni ya wananchi waliozungumza kwa uchungu kuhusu rasilimali za nchi, hivyo miswada hiyo inahitaji muda wa kutosha wa kuijadili kwa maslahi ya Taifa.

  JAPHET HASUNGA
Mbunge wa Vwawa (CCM), Japhet Hasunga, alisema miswada hiyo ya maliasili ni muhimu na hawawezi kusubiri muda wa kutosha kwa kuwa Tanzania imeibiwa vya kutosha.

  MANSOOR HIRANI
Mbunge wa Kwimba (CCM), Mansoor Hirani, alisema serikali ichukue migodi yote ambayo ina zaidi ya miaka 20 kwenye uzalishaji kwa kuwa wamepata faida ya kutosha.

  SERUKAMBA
Mbunge wa Kigoma Kaskazini (CCM), Peter Serukamba, alisema miswada hiyo ni mapinduzi ya kiuchumi huku akimtaka Waziri wa Katiba na Sheria, Prof. Palamagamba Kabudi, kutoshawishika na wakubwa duniani watakaolalamikia sheria hizo na kutaka kufanyiwa marekebisho.