Mchezaji Daga Shenko ambaye msimu uliopita alicheza Africans Lyon amesema timu yake ya Tandavamba inamlipa shilingi laki moja kila anapocheza mechi ya Ndondo Cup.
Tandavamba inayotokea maeneo ya Kigamboni, ilipata ushindi wa 2-1 dhidi ya Temeke Squad kwenye mchezo wao wa pili wa Kundi D uliochezwa kwenye uwanja wa Kinesi.
“Nilikuwa nacheza timu hii tangu zamani kwenye mashindano ya mitaani ndio maana hadi sasa hivi wameamua kuendelea kubaki na mimi kwenye mashindano ya Ndondo Cup.”
“Wananilipa shilingi laki moja (100,000) kwa kila mechi, sina mkataba nao lakini kila mechi inapomalizika wananipa hela yangu maisha yanaendelea.”
Daga alifunga magoli mawili kwenye mchezo wa Tandavamba dhidi ya Temeke Squad na kuisaidia timu yake kupata pointi tatu na kufikisha pointi nne kwenye Kundi D sawa na Boom FC baada ya timu za kundi hilo kucheza mechi mbili, Boom inaongoza Kundi D kutokana na wastani mzuri wa magoli.
Mshambuliaji huyo kwa sasa amesaini mkataba wa kucheza Kagera Sugar kuanzia msimu ujao wa ligi kuu Tanzania bara itakayoanza mwezi Agosti mwaka huu.