SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Ijumaa, 23 Juni 2017

T media news

TAMKO RASMI LA KUMPONGEZA MH. RAIS JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI KWA HATUA YA UJASIRI YA KULINDA RASILIMALI ZA NCHI YETU.

Sisi Umoja wa Wazee kata ya Nyamuswa, tukiwawakilisha Wazee wa Ikizu tunakupongeza Mheshimiwa Rais John Pombe Joseph  Magufuli kwa ujasiri wa uamzi mkubwa na mgumu wa kujitoa mhanga kutetea Rasilimali za nchi hasa #Madini.

Tunatambua kuwa, haikuwa kazi rahisi kufikiri na kuamua kuchukua hatua ya kuzuia usafirishaji wa Makontena ya #Makinikia yaliyokuwa yakisombwa  kiholela na kinyemela na wezi wa nje ya nchi kwa jina la wawekezaji huku wakisaidiwa na watanzania wachache wasio waadilifu.

Tunatambua kuwa haikuwa kazi rahisi ya kuchukua uamuzi wa kuunda Kamati ya Wataalam wa Miamba na Madini na Kamati ya Uchumi na Sheria ili kupata ukweli.
 Sisi Wazee wa Ikizu tunatambua kuwa vita hii uliyoianzisha wewe Mheshimiwa Rais hapa Tanzania sio ndogo dhidi ya Mabepali wa kiuchumi duniani. Tunajua vita hii  ni vita ya ukombozi wa pili wa Nchi yetu ili kujikwamua kiuchumi.

Sisi Wazee wa Ikizu, Sehemu ya Tanzania, Tunakupongeza kwa namna ulivyo jitofautisha katika utendeji wako kwa kugusa maisha ya wanyonge katika nyaja mbalimbali tangu umekuwa Rais Oktoba 2015.
Sisi tunakuunga mkono kwa kuwa umegusa KIU ya Watanzania ya kulinda Rasimali zao dhidi ya majangili na waporaji wasio na aibu kwa jina la wawekezaji, Umedhihirisha kuwa wewe ni KIJANA Mzalendo wa  Nchi hii jina lako litakumbukwa Vizazi na Vizazi kama mtangulizi wa Taifa Mwalimu #JULIUS_KAMBARAGE_NYERERE.

Sisi wazee wa Ikizu,Kwa umoja wetu tunakuunga mkono kwa kazi hii uliyoianza ambayo baadhi yetu wasio na aibu walijaribu kutisha kwamba tutawekewa vikwazo Duniani na kushitakiwa katika Mahakama za Kimataifa lakini wamepatwa na aibu baada ya hao waporaji kutubu na kukubali kulipa wizi wote waliotusababishia.

Sisi Wazee wa Ikizu – Nyamuswa tunakuombea Afya, Uwezo na Hekima zako ziongezeke maradufu katika kusimamia Nchi. Hakika tunaona  #DIRA ya Nchi kupitia wewe kwa huduma tunazopata na Dunia nzima inavyotusifu sisi kama Tanzania.

Sisi Wazee wa Ikizu tuko nawe bega kwa bega, Usiogope, Kivuli chetu kiko nyuma yako “ Our shadow is next to yours” na Mungu yuko juu yako atakulinda kwa kila jambo uiongoze nchi salama.

Eneo letu hili la Ikizu linakubariki na kukukaribisha ututembelee ujionee Historia ya baraka tulizozitoa kwa watangulizi wenzako enzi na enzi, Sisi wazee wa Ikizu ndiyo tuliyo msaidia Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kuanza kutengeneza katiba ya TANU kupitia Chifu wa Waikizu Mohamed Makongoro Matutu.

Sisi Waikizu ndiyo tuliyemtolea ushahidi Mwalimu Nyerere kwa kesi ya mkoloni ya uchochezi na uanzishwaji wa chama cha Siasa na tukashinda.

Sisi Wazee wa Ikizu ndiyo tuliochonga  #FIMBO ya Mwalimu Nyerere aliyokuwa akitembea nayo kote Duniani,   Fimbo hii hutolewa kwa watu Maalumu walifanya mambo makubwa na uongozi unaokubalika.

Sisi Wazee wa Ikizu leo tunajivunia kukuunga mkono kwani hata waanzilishi kumi (10) wa mwanzo wa chama cha TANU wanne  walitoka eneo letu la Ikizu hao ni Mzee  Kisung’uda Kapera, Abubakari Iranga, Suleman Kitwara na Kibiriti  Miyasi. Hawa waliazisha TANU na kumsaidia Mwalimu Nyerere kuongoza Chama na baadaye kupata uhuru 1961.
Kupitia historia hiyo ya eneo letu la Ikizu, nasi leo tunakuunga mkono Rais wetu uendelee kupambana na wahujumu Uchumi, Mafisadi, Wala rushwa , Wavivu na wasiopenda maendeleo ya nchi yetu. Hakika tumeona utaacha historia kubwa katika PAJI la nchi yetu.

Tunakupongeza sana kwa hatua na mafanikio uliyofikia ya kulinda Rasilimali za Nchi yetu, Penya kila kona uokoe na mengine mengi ambayo kama nchi tuliyapuuza ili hali ni mambo muhimu kwa ustawi wa watu wote.

Hongera sana wewe Rais, Makamu wa Rais, Waziri mkuu na timu yako ya kazi kwa kasi na umakini wa uongozi, Uzalendo na ujasiri mlionao katika kuijenga nchi yetu. Endelea, Usiogope, Usirudi nyuma sisi tuliokuchagua tupo na tunakuunga mkono.

KARIBU IKIZU, Uone eneo ambalo Mwalimu Nyerere alitumia kukaa na kuandika KATIBA YA TANU, Uone wazee waliochonga fimbo ya Mwalimu Nyerere na  uone historia ya Wazee wapenda maendeleo na jitihada za kuunga juhudi za maendeleo.

Pokea zawadi ya #FIMBO ishara ya upendo wetu na ishara ya kukubalika kwa uongozi wako.
Mungu akubariki sana Mheshimiwa Rais wetu, Akupe afya njema, Hekima na uwezo wa kuongoza Nchi salama salimini.

_____________________________________________

IMEANDALIWA NA UMOJA WA WAZEE MFUKO WA MAENDELEO KATA YA NYAMUSWA– IKIZU
BUNDA,
MARA.
23/06/2017