SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumatano, 17 Mei 2017

T media news

Watumishi wa umma UDSM wakutwa na vyeti feki

Sakata la vyeti feki vya kielimu na taaluma kwa watumishi wa umma limekikumba pia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), baada ya watumishi wake 24 kufukuzwa kazi kwa kubainika kuwa na vyeti feki, huku wengine 128 vyeti vyao vikiwa na utata.

Makamu Mkuu wa UDSM, Profesa Rwekaza Mkandala alieleza kuwa tangu kazi ya ukaguzi ilipoanza katika chuo hicho mwaka jana, watumishi 24 walibainika wakitumia vyeti vya bandia na 128 vyeti vyao vina utata.

Alisema idara ambazo watumishi wake walibainika wakutumia vyeti feki ni polisi, madereva, mapokezi, na watumishi wa kada ya chini.

“Kazi ya uhakiki mbona ilishakamilika muda mrefu? Watumishi 24 walibainika wana vyeti feki na wengine 128 vyeti vyao vina utata, na idara zilizobainika ni hizi ndogo ndogo,”alisema Profesa Mkandala.

Alipoulizwa ni kwa namna gani watumishi 128 vyeti vyao vina utata, Prof. Mkandala alisema baadhi havionekani katika mfumo wa Baraza la Taifa la Mitihani (Necta).

Alisema UDSM bado inaendelea kuvifanyia uchunguzi vyeti hivyo na iwapo itabainika kuwa ni vya kughushi nao watafukuzwa kazi.

Kazi ya uhakiki wa vyeti vya elimu na taaluma kwa watumishi wote wa umma ilianza Machi mwaka jana lengo kuu likiwa ni kuongeza ufanisi katika kazi ya kuwatumikia Watanzania pamoja na kutoa nafasi za ajira kwa Watanzania wenye sifa kitaaluma.

Tangu kuanza kwa ukaguzi huo, zaidi ya watumishi 9,932 walibainika wakitumia vyeti bandia wakiwamo waliokuwa wakihudumia taasisi nyeti kama Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) ambayo watumishi wake 134 walikutwa na vyeti feki.

Baada ya kupokea taarifa ya ukaguzi iliyobaini watumishi hao karibu 10,000 mwezi uliopita, Rais Magufuli alimwagiza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora), Angela Kairuki, kuwatangazia waondoke mara moja katika nafasi zao za kazi kabla ya Mei 15, vinginevyo wangechukuliwa hatua kali za kisheria, sambamba na kutangaza nafasi mpya za ajira.

Hadi sasa inaelezwa kuwa ofisi mbalimbali za Serikali zimekuwa na upungufu wa watumishi baada ya wafanyakazi hao kubainika wakitumia vyeti bandia.