Makamu wa Rais wa klabu ya Simba Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ amethibitisha kwamba, mchakato wa mabadiliko kwa klabu ya Simba upo palepale licha ya kusaini mkata wa udhamini na kampuni ya SportPesa.
Wasiwasi ulitanda ndani ya wanachama na wadau wa klabu hiyo huenda mkataba wa miaka mitano waliosaini Simba na SportPesa ungezima mchakato wa mabadiliko ambao tayari umeshafikia sehemu nzuri kwa sasa.
“Kitu kikubwa ambacho naweza kuwaambia wana Simba ni kwamba, hapa kuna vitu viwili, uwepo wa wadhamini ndani ya klabu ya Simba ambacho ni kitu muhimu kwa sasa lakini jambo la pili ni mchakato wa mabadiliko ili kubadilisha umiliki na uendeshaji wa klabu yetu,” amesema Kaburu wakati akizungumza na Clouds FM.
“Udhamini utasaidia sana uendeshaji wa kila siku wa klabu lakini haya masuala ya maadiliko ndio yataleta uwekezaji. Tumeona kwa muda mrefu tumekua tukijaribu kucheza mpira, kulipa mishahara na mambo mengine lakini tumeshindwa kufanya uwekezaji wa miundo mbinu kama uwanja na vitu vingine.”
Mei 12, 2017 uongozi wa Simba ulisaini mkataba wa miaka mitano wa udhamini na SportPesa wenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 4.9 za Tanzania hali iliyozua wasiwasi kwa baadhi ya wadau wa soka nchini huenda mchakato wa mabadiliko ndio ukawa umefika mwisho.