WAZIRI wa Maji na Umwagiliaji, Gerson Lwenge, amesema kauli ya Mbunge wa Misungwi, Charles Kitwanga (CCM), aliyoitoa bungeni wiki hii, kwamba kama Serikali haitapeleka maji atahamasisha wananchi wakang’oe mtambo wa maji ulioko jimboni kwake, ni sawa na uasi.
Kutokana na kauli hiyo, amemtaka Kitwanga ahame chama kama haoni jitihada za kupeleka maji jimboni kwake zinazofanywa na Serikali.
Lwenge alitoa kauli hiyo bungeni juzi, alipokuwa akihitimisha mjadala wa bajeti ya wizara yake kwa mwaka wa fedha wa 2017/2018.
“Spika, naomba nizungumzie mchango wa Kitwanga, ambaye alichangia hapa kwa hisia kubwa akionyesha Serikali ya CCM haijafanya chochote kwenye Wilaya ya Misungwi,”alisema na kuongeza:
“Nataka nimuulize Kitwanga kama yupo hapa, kwamba hayo ni maneno yake au ni maneno ya wananchi? Kama ni maneno ya wananchi, nitawaambia ni nini kimefanyika Misungwi kwa sababu hata juzi tumesaini mikataba ya maji ya shilingi bilioni 38 kutoka Ziwa Victoria kwenda Misungwi na Mwenyekiti wa Halmashauri alikuwepo.
“Kitwanga anaposema atakwenda kuhamasisha wananchi wakabomoe mtambo wa Iherere maana yake analeta uasi au hathamini kazi iliyofanywa na chama chake?
“Kama ni hivyo, sasa ajitoe kwenye chama kwa sababu Serikali imepeleka fedha na kwa maendeleo yaliyofanyika, ni lazima tuwahamasishe wananchi kutunza miundombinu iliyopo badala ya kwenda kuibomoa. Hata kwenye umeme huwa tunaona wanaweka kwenye kijiji kimoja na kuruka hadi kijiji cha nne, lakini hatujawahi kuona wanang’oa nguzo.”
“Kwa hiyo, nataka nimwambie kwamba, Serikali itaendelea kuboresha maji katika maeneo mbalimbali, ikiwamo Misungwi na Usagara.”
Lwenge alisema kwa upande wa Usagara, Serikali itapeleka maji yanayosukumwa kutoka Nyashishi, ambapo lita milioni tatu zitazalishwa na usanifu unafanyika Buswelu.
“Sasa akisema haungi mkono bajeti maana yake hizi fedha tuzitoe tupeleke wilaya nyingine,” alisema.
Pamoja na maelezo hayo, Lwenge alisema wizara yake kupitia Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mwanza, imesaini mkataba wa Sh bilioni 38 kwa ajili ya kupeleka maji Misungwi na kazi hiyo imefadhiliwa na Benki ya Ulaya na Shirika la Maendeleo la Ufaransa.
Wakati huo huo, alisema Sh bilioni 3.5 zitatumika pia kupeleka maji katika vijiji mbalimbali vilivyopo wilayani Misungwi.
Majibu hayo ya Lwenge aliyompa Kitwanga, ambaye alikuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi kabla uteuzi wake haujatenguliwa mwaka jana na Rais Dk. John Magufuli, ni mwendelezo wa kauli zinazotolewa na wabunge wa CCM baada ya kutoridhishwa na mchango wa mbunge mwenzao huyo.
Aliyeanza kumshambulia Kitwanga ni Mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Msukuma (CCM), ambaye wiki hii alilitaka Jeshi la Polisi likampige mabomu Kitwanga na wananchi watakaoandamana kwenda kung’oa mtambo wa maji.
“Jana nilisikiliza mchango wa Kitwanga akilalamika kwamba atahamasisha wananchi 10,000 wa Misungwi ili wakazime mashine ya maji Iherere,” alisema na kuongeza:
“Nilisikitika sana na nataka niwaulize kwamba, nyinyi mawaziri wa Magufuli hivi vile viapo mnavyokula mnajua maana yake?”
“Kama hamjui maana ya hivi viapo, basi sina hakika kama mko sawasawa na kama hamko sawaswa, Ndalichako (Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi), hebu pitisha operesheni ya vyeti feki huenda hapa penyewe kuna feki za kutosha.”
“Hivi inawezekana vipi mtu uliyekuwa waziri unasimama hapa na kusema ulipokuwa waziri ulikuwa umebanwa kuzungumza na baada ya kufukuzwa sasa uko huru kuzungumza?”