Bado soka letu limefunikwa na wingu la kishirikina kuliko maandalizi na kucheza kwa mbinu za kuwapatia ushindi uwanjani. Leo baada ya mchezo wa ligi kuu Tanzania bara kati ya Yanga na Toto Africans shaffihdauda.co.tz imekumbana na vitu vinavyoashiria imani za kishirikina (uganga au uchawi).
Licha ya kwamba imani za kishirikina kutotambulika na shirikisho la soka Duniani FIFA, kunabaadhi ya timu zimekuwa zikiamini katika mafanikio yatokanayo na imani za kishirikina.
Leo Mei 16, 2017 mara baada ya Yanga kupata ushindi wa goli 1-0 dhidi ya Toto, vilikutwa vitu kwenye chumba cha kubadilishia nguo cha Toto Africans ambavyo vinahushwa na imani za kishirikina. Kulikuwa na hirizi mbili za karatasi nyeupe zilizofungwa kwa uzi mweusi pamoja na chupa moja ya maji ambayo ilikuwa na karatasi mbili.
Karatasi moja ilikuwa imeandikwa kwa wino wa blue maandishi ambayo yanasomeka neno ‘KOMBE’ lakini ndani ya hiyo karatasi kulikuwa na karatasi nyingine nyeupe ambayo haikuandikwa kitu. Cha ajabbu ama kushangaza ni kwamba, maji yaliyokuwa kwenye hiyo chupa yalikuwa na rangi nyekundu.
Shaffihdauda ilishuhudia mtu mmoja akizifungua hirizi mbili ambazo ndani yake kulikuwa na maandishi hakuna aliyeelewa maana yake lakini inaamika yalikuwa ni ya lugha ya Kiarabu.
Hivi karibuni alionekana komando wa klabu ya Simba akimwaga vitu mithili ya unga kwenye moja ya goli la uwanja wa taifa kabla ya kuanza kwa mchezo wa nusu fainali ya kombe la FA dhidi ya Azam FC. Kumekuwa na matukio mengi ya baadhi ya timu kugoma kuingia kwenye vyumba vya kubadilishia nguo kutokana na imani za kishirikina lakini kuna baadhi ya timu zimekuwa zikilalamika kupuliziwa hewa ya sumu kwenye vyumba vyao.
Mara kadhaa pia timu zimepigwa faini na kupewa onyo kali na TFF kwa kutumia milango isiyo rasmi kwamadai ya kukwepa hujuma za kichawi.