SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumamosi, 15 Aprili 2017

T media news

TRA Waja na Mbinu Mpya ya Kuwabana Wakwepa Kodi Kupitia Mashine ya EFD...!!!


MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA), imeendelea kuwabana wala rushwa na wanaoghushi risiti za ukusanyaji maduhuli kwa kuboresha mfumo wa kieletroniki wa utumiaji wa mashine za (EFD) utakaowezesha miamala na risiti kuwa na saini za kieletroniki.

Kaimu Kamishna Mkuu wa TRA, Neema Mrema, aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akifungua mafunzo kwa ajili ya taasisi na mashirika ya umma.

Mrema alisema hivi karibuni mawakala wa mashine za kieletroniki za kutumia risiti watawafungia mfumo huo taasisi na mashirika hayo ili wakusanye maduhuli kupitia mashine hizo.

Aidha, alisema TRA imefanya mabadiliko katika mfumo wa usimamizi wa matumizi ya mashine za kieletroniki za utoaji risiti (EFDMS) pamoja na mashine za EFD ili kupunguza gharama kwa serikali.

Alisema mfumo huo wa kielektroniki utaipunguzia serikali gharama za kununua mashine halisi kwa kuwa umeunganishwa na mfumo wa kuhifadhi taarifa wa TRA.

“Una usalama wa hali ya juu kwani miamala na risiti zote itakuwa na saini ya kieletroniki … hivyo kunapunguza uwezekano wa kughushi risiti kutoka kwenye mashine ambazo hazijasajiliwa na mfumo wa TRA,” alisema.

Pia alisema mfumo huo ni wa kiintelejensia kutokana na kuwa na uwezo wa kutambua hati ya mauzo kwa mkopo, marejesho ya mauzo, risiti halali na za kudurufu.

Kadhalika, alisema mfumo huo ni rafiki na unaweza kuunganishwa na mifumo mingine kama ya ankara, mauzo na stakabadhi kwa kufanya mabadiliko machache na una ruhusu matumizi ya fedha mbalimbali.

Aliongeza kuwa mfumo huo ni wa uwazi kwa sababu ukomo wa kila risiti unahakikiwa na una uwezo wa kutambua huduma kama imetolewa au la.

Kuhusu kodi ya zuio iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2013, kamishna huyo alisema imekuwa na changamoto kwa idara na taasisi za serikali kutokana na wahusika kukosa uelewa wa kutosha wa utozaji wa kodi husika.

“Kumekuwa na mkanganyiko kati ya utozaji wa kodi ya zuio ya asilimia mbili katika usambazaji wa bidhaa kwa Idara na taasisi za serikali zinazotegemea bajeti ya serikali kuu kwa asilimia 100 na ile ya asilimia tano kwa huduma,” alisema.

Alisema kupitia mafunzo hayo washiriki wataelimishwa kuhusu mabadiliko ya sheria fedha ya mwaka 2016, sheria ya kodi ya ongezeko la thamani ya mwaka 2014, kodi ya zuio katika bidhaa na huduma na mfumo huo wa ukusanyaji maduhuli.

Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi TRA, Richard Kayombo, alisema utumiaji wa risiti za kawaida umekuwa ukitoa mianya ya upoteaji wa mapato hivyo kupitia mafunzo hayo wanaamini washiriki watatambua wajibu wao katika kuhakikisha makusanyo yanaongezeka.

Mhasibu Mwandamizi kutoka Bodi ya Sukari Tanzania, Devotha Sanga, alitaja changamoto wanazokumbana nazo kuwa ni kushindwa kutambua viwango vinavyotakiwa kutozwa kwa mtu binafsi au kampuni kupitia kodi ya zuio ni asilimia ngapi.

Pia alisema katika kodi ya ongezeko la thamani kumekuwa na changamoto ya risiti za kughushi ambazo wanashindwa kuzitambua.