Msanii wa filamu nchini, Steve Nyerere ambaye pia aliwahi kuwa mwenyekiti wa Bongo Movie Unit, amedai kitendo cha waigizaji kujiingiza kwenye siasa ni chanzo cha tasnia ya filamu nchini kupoteza mvuto.
Amesema hayo ikiwa ni siku chache tangu kufanyika maandamano ya baadhi ya wasanii wa filamu kuishinikiza serikali kuwaondolea kodi katika filamu zao au kuhakikisha inakusanya pia kodi za filamu za nje ambazo zinakuwa zinapakuliwa katika mitandao kitu kinachopelekea kuua soko la ndani la filamu za Bongo.
“Mimi naomba niongee ukweli leo, kilichotuawa Bongo Movie ni siasa. Kipindi tupo kwenye uchaguzi mkuu kulikuwa na makundi mawili ya siasa ambayo yalikuwa yanawasapoti wagombea tofauti ndani ya tasnia ya filamu,” Steve Nyerere alikiambia kipindi cha Planet Bongo cha EA Radio.
Aliongeza,
“Lakini cha kushangaza uchaguzi tumeumaliza vizuri ila badala ya kuendelea na kazi zetu za uzalishaji wa filamu bado tunaendeleza kazi za watu ambazo hatuna hata utaalamu nazo,”
Pamoja na hayo Steve Nyerere ameongeza wapo wasanii wa filamu ambao wameweza kutenganisha siasa na filamu na kwamba hao ni wale ambao wamebahatika kuvaa kofia hizo mbili ndio maana wametumia busara zao kutotumika kwenye maandano ya watu wachache.
“Unajua pamoja na siasa kuna watu pale Bongo Movie wana kofia mbili mbili mfano mimi niliwahi kugombea Ubunge wa Kinondoni kwa hiyo lazima najua nini nafanya, Irene Uwoya ni Mbunge pale na anayo nafasi yake ndani ya chama ikitokea bahati mbaya mbunge wa viti maalumu akaanguka yeye ndiye atakayeziba pengo au Wema Sepetu na harakati aliozonazo sasa hivi na ndio maana hata ukiangalia kwenye maandamano watu waliyoyafanya wao walikaa pembeni siyo kwamba siyo wasanii , hapana ni wasanii ambao wamejitambua na hawataki kutumika kwa maslahi ya watu wachache,” Steve alifafanua.