Mbunge wa jimbo la Mtama mkoani Lindi kupitia tiketi ya CCM, Nape Moses Nnauye ametoa ya moyoni kwa kusema kila akiyakumbua maisha aliyoyashuhudia wakati akizunguka mikoa mbalimbali kwa miezi 38 ndiyo yanamfanya aonekane mkorofi kila mara anapoyakumbushia.
Nape ameyasema hayo kupitia yale aliyoyaandika kwenye ukurasa wake rasmi wa Twitter kuwa akikukumbuka maisha magumu aliyowaona wananchi wakiishi anaonekana ni mkorofi mara zote akikumbushia. Kupitia Twitter, aliandika, “Niliyashuhudia maisha haya mikoani(38months),nadhani ndio nikiyakumbuka naonekana mkorofi!!Iko haja kama Taifa kuangalia vipaumbele vyetu!”
Kauli ya Nape kuwa taifa liangalie upya vipaumbele vyake inaweza kutafsiri kuwa kutazama picha hiyo kuwa wananchi wana shida ya maji safi na salama, huduma za afya na vitu vingine muhimu zaidi kwa maisha yao.
Lakini pia Nape alichapisha picha nyingine ambayo inakumbushia kipindi cha miezi 38 alichozunguka nchi nzima kuipigia debe CCM huku akimpongeza Katibu Mkuu wa Chama CCM, Abdulrahman Kinana kwa kazi kubwa na ngumu aliyofanya.
Baadhi ya watu wamemkosoa kiongozi huyo sababu anaonekana analalamika kwa vile alivuliwa uwaziri na kuwa ndiyo sababu ya kueleza haya yote. Lakini yeye amekanusha hayo na kusema kuwa hajaanza kuyashughulikia, au kuyazungumzia mambo haya mara tu alipoenguliwa kwenye uwaziri.
Lakini pia watumiaji wengine wa mitandao wamemtaka Nape kupeleka matatizo hayo bungeni badala ya kuyaandika kwenye mitandao ya kijamii kwani si sehemu sahihi ya kuelezea matatizo hayo.