Katika kile kinachoonekana kuwa Kiongozi wa Korea Kaskazini, KIM JONG UN, haogopi chochote na yuko tayari kukabiliana na uvamizi wa Marekani, kiongozi huyo leo tarehe 15.04.2017 ameonesha makombora mapya katika Gwaride Maalum la Kumbukumbu ya 105 ya kuzaliwa kwa mwasisi wa taifa hilo la kikomunisti, KIM IL SUNG, ambaye pia ni babu yake.
Makombora yaliyooneshwa kwa mara ya kwanza leo ni yale ya kurushwa kutoka kwenye nyambizi, yaani submarine-launched ballistic missiles, na makombora ya masafa marefu (ICBM).
Makombora ya kurushwa kutoka kwenye nyambizi, aina ya Pukkuksong-2 submarine-launched ballistic missiles (SLBMs), yalipitishwa mbele ya Kim Jong Un katika malori maalum kwa mara ya kwanza huku kiongozi huyo, akiwa amevalia suti nyeusi, shati jeupe na tai, akiyapungia.
Afisa mmoja wa ngazi za juu wa serikali ya Kim Jong Un anayeitwa CHOE RYONG HAE, akiwahutubia askari katika gwaride hilo, amemlaumu Rais DONALD TRUMP wa Marekani kwa kuanzisha hali ya vita katika rasi ya Korea na kuahidi kuwa watajibu ubabe wa Marekani kwa vita kamili. Afisa huyo alisema: "Tutajibu vita kamili kwa vita kamili na vita vya nyuklia kwa shambulizi la nyuklia kwa mtindo wetu", amenukuliwa na shirika la habari la AP