Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe ameilaumu Serikali kuu kwa kutoa asilimia 15 pekee ya fedha kati ya Sh9 bilioni zilizopitishwa kwenye bajeti ya Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji ya mwaka 2016/2017.
Akizungumza na wakazi wa Kata ya Gungu mjini humo, Zitto amesema kutokana na hali hiyo hakuna kinachoweza kufanyika wilayani humo.
“Ndiyo maana tunawaomba wananchi wapuuzeni wapinzani wetu wanaolalamika kwamba hatujatekeleza ahadi zetu,” amesema Zitto.
Mbunge huyo amewataka wananchi kufanya kazi za uzalishaji mali ili kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja.
“Fanyeni kazi ili muongeze kipato chenu, msitegemee kwamba kuna mtu au kiongozi atakayewaletea fedha mifukoni, kila mmoja afanye kazi halali ya kuwaingizia kipato,” amesema.
Mkazi wa mjini Kigoma, Geofrey Masao amesema Serikali inatakiwa kupeleka fedha za miradi kwa wakati katika halmashauri ili kuziwezesha kutekeleza wajibu wake.
“Tutawalaumu tu wawakilishi wetu bila sababu za msingi kumbe Serikali ndiyo inayostahili lawama hizi. Hizi ni fedha zetu za kodi tunataka zije zitutumie,” amesema Masao.