WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametembelea kiwanda cha sukari cha Kampuni ya Alteo ya Nchini Mauritius chenye uwezo wa kukamua tani 400 za miwa kwa saa na kuzalisha tani 170,000 za sukari kwa mwaka.
Kampuni ya Alteo inamiliki kiwanda cha sukari cha TPC mkoani Kilimanjaro kwa ubia na Serikali ya Tanzania na kinazalisha tani 110,000 kwa mwaka.
Waziri Mkuu ametembelea kiwanda hicho leo (Jumanne, Machi 21, 2017) na kujionea namna wanavyozalisha sukari kwa kutumia teknolojia ya kisasa.
Aidha, Waziri Mkuu amefanya mazungumzo na uongozi wa kiwanda hicho na kuwashawishi waongeze maeneo ya uwekezaji nchini.
“Tekonolojia wanayoitumia katika uendeshaji wa kiwanda chao ni nzuri hivyo tumewashawishi waje kuongeza maeneo ya uzalishaji wa sukari nchini ili tuweze kukidhi mahitaji,” amesema.
Waziri Mkuu amesema Tanzania kuna viwanda vitano vya sukari ambavyo ni Mtibwa, Mahonda (Zanzibar), TPC, Kilombero na Kagera vinavyozalisha tani 320,000 kwa mwaka huku mahitaji ni tani 420,000.
Kwa upande wake Waziri wa Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dkt. Khalid Salum Mohammed amesema Zanzibar kuna kiwanda kimoja cha sukari ambacho uzalishaji wake haukidhi mahitaji kutokana na
uhaba wa malighafi.
Kutokana na hali hiyo, Dkt. Khalid ameikaribisha kampuni ya Alteo kwenda Zanzibar kushirikiana na Serikali katika uwekezaji hususani kwenye viwanda vya sukari. Naye Mtendaji Mkuu wa Kampuni hiyo Bw. Patrick de Labauve amesema wamekubali kuongeza maeneo ya uwekezani wa mashamba ya miwa nchini.
Pia ameomba Serikali iwapatie fursa ya uwekezaji katika sekta ya utalii mkoani Kilimanjaro. “ Kuna vivutio vingi vya utalii ukiwemo mlima Kilimanjaro,”.
Akizungumzia kuhusu ajira amesema kiwanda cha TPC kimeajiri wafanyakazi 3,000 wakiwemo 1,900 wa kudumu.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMANNE, MACHI 21, 2017.