Na Immaculate Makilika- MAELEZO
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dk. Augustine Mahiga amefanya mazungumzo na mjumbe maalum wa Kansela wa Ujerumani Angela Merkel, Balozi Harro Adt, ambapo alipokea, niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli, ujumbe maalum kutoka kwa Kansela Markel.
Akizungumzia ziara ya Balozi Adt nchini, Balozi Dk. Mahiga alisema kuwa “Kansela Merkel amemtuma Balozi Adt, kuleta ujumbe maalum ambao ni ombi kwa Rais Magufuli la kuisaidia Ujerumani katika kugombea nafasi ya kuwa mjumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wakati wa uchaguzi wa nafasi hiyo unaotarajiwa kufanyika mwaka 2018”.
Balozi Dk. Mahiga alieleza kuwa dhamira ya Ujerumani ya kugombea nafasi hiyo ni kusaidia mageuzi ndani ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ikiwa ni pamoja na kuridhia nchi za Afrika katika mchakato wa kupokea nafasi mbili za kudumu katika baraza hilo. Nchi nyingine zinazogombea nafasi hizo ni Israel na Ubelgiji.
Balozi Mahiga alisema kuwa, Ujerumani imeahidi masuala kadhaa kama vile kusimamia amani katika jumuiya ya kimataifa na katika ukanda wa Afrika, kusimamia haki za binadamu katika ngazi ya dunia na kuendelea kuimarisha uhusiano wake na nchi nyingine.
Aidha, Ujerumani imesisitiza nia yake ya kuunga mkono mageuzi mapya katika bara la Afrika ambayo yataikomboa Afrika na kuleta maendeleo zaidi barani humu.
Katika mazungumzo hayo, Balozi Dk. Mahiga alisema kuwa ameiomba Ujerumani isaidie ujenzi wa jengo mahususi la mahakama ya Afrika iliyopo mjini Arusha ikiwa ni pamoja na kuboresha mfumo mzima wa mahakama barani Afrika pamoja na kuisaidia Afrika katika kupambana na masuala ya mabadiliko ya tabianchi.
Kwa upande wake, mjumbe maalum kutoka Ujerumani Balozi Adt, alisema kuwa amefurahishwa na mapokezi aliyoyapata alipowasili nchini.
Aidha, Mjumbe huyo Maalum wa Kansela wa Ujenrumani alieleza matumaini yake kuwa Tanzania ambayo ni rafiki wa Ujerumani kihistoria itatoa msaada juu ya nafasi hiyo ili kusaidia kutekeleza malengo waliojiwekea kiufanisi kuhakikisha Afrika inapata nafasi mbili za kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Uhusiano kati Tanzania na Ujerumani ni wa kihistoria na wakati wote nchi mbili hizo zimekuwa zikifanya kila jitihada za kuuimarisha.
Chini ya uhusiano huo, Ujerumani imekuwa ikiisaidia Tanzania katika sekta mbalimbali za maendeleo kama vile elimu, miundombinu na wanyamapori.
MWISHO.