KIONGOZI wa dini ya kiislamu, dhehebu la Shia, Shehe Hemed Jalala amesema kuwa wataendelea kutambua na kuthamini nafasi ya mwanamke katika jamii kwa kuwapatia haki zao wanazostahili.
Shehe Jalala alisema kuwa mwanamke ni mtu muhimu katika kuchangia maendeleo ya familia na taifa na kwamba dini hiyo inatoa kipaumbele katika kuwapa haki zao.
Aliyasema hayo jana kwa waandishi wa habari kuhusu maadhimisho ya kuzaliwa kwa Bi Fatma mjukuu wa Mtume Muhammad (S.A.W) aliyezaliwa mwaka 615 AD.
Alisema kuwa siku hiyo ni muhimu wanapomuenzi mwanamke aliyefanya mambo makubwa katika dini hiyo ikiwa ni pamoja na kuhibiri habari njema.
"Ikumbukwe kuwa zamani wanawake hawakuruhusiwa kuingia kwenye nyumba za ibada lakini Mtume alimuonesha mwanamke ni kama mtu mwingine kwa kufundisha usawa na kutoa haki kwa wanawake na wanaume," alisema Shehe Jalala.
Alifafanua kuwa mwanamke amekamilika kama alivyo mwanaume kwani ndiye anatengeneza umma, watu na wanaume wanaoleta maendeleo katika jamii na kusisitiza kuwa penye maendeleo ya mwanaume nyuma yake yupo mwanamke.
"Kumekuwa na maneno kuwa uislamu una aina fulani ya dhuluma kwa mwanamke, la hasha anapatiwa haki zake zote anazostahili ikiwemo haki ya kuzungumza mbele ya watu kufuata misingi ya dini. Bi Fatma alienda kwenye msikiti na kutoa hutuba mbele za watu," alisema
Aliongeza kuwa mwanamke anayo haki ya kurithi, haki ya kuongoza, haki ya kufanya kazi mbalimbali kwa kuzingatia maslahi na heshima yake kwa misingi ya dini na sheria