Hii ilikuwa stori lakini haikuandikwa! Mwimbaji wa Nyimbo za Injili Bongo, Emmanuel Mbasha amefichua jambo kwa kueleza kwamba, aliyemmuingiza yeye pamoja na mtalaka wake, Flora Mbasha katika masuala ya siasa, alikuwa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Pombe Magufuli.
Akizungumza katika mahojiano maalum na Risasi Jumamosi, Mbasha alifunguka kuwa, Rais Magufuli alimpigia simu akiwa studio kama alivyomfanyia staa wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond’ hivi karibuni, Clouds TV.
Mbasha alifunguka mambo mengi lakini suala zima la historia yake kisiasa, alisema Rais Magufuli ndiye ilikuwa chachu ya yeye na Flora kujiunga na Chama Tawala, Chama cha Mapinduzi (CCM). “Nakumbuka ilikuwa ni mwaka 2005, nilikuwa na aliyekuwa mke wangu, Flora. Tulienda Clouds FM, wakati huo walikuwa kule Kitega Uchumi, Posta.
Tulikuwa tumeenda kutambulisha wimbo wetu, nakumbuka ulikuwa ni ule Tanzania, sasa baada ya Kipindi cha Gospo Track kuishia, Mtangazaji George Njogopa alinitaka niseme namba ili wadau waweze kutusaidia.
“Nikataja namba zangu hewani. Sasa kama nusu saa hivi mbele baada ya kipindi kuisha, sisi tulikuwa tunashuka ghorofani, ghafla nikasikia simu inaiita. “Nikapokea, aliyepiga alijitambulisha kwa jina la John.
Akaniambia kuwa hayupo Dar, ila akirudi atanitafuta ili aweze kunisaidia,” alisema Mbasha.
Mbasha alisema hakuwa na imani kama kweli John atamtafuta tena na hakujua pia alikuwa anataka kumsaidia kivipi, lakini kama zari, baada ya wiki kupita, alipigiwa simu na kuambiwa aende Posta.
“Yaani sikuamini, John akapiga simu, akatuelekeza twende Posta, nikashangaa anatuambia tuingie Wizara ya Ujenzi. Tukaingia, akatuambia tumuambie mlinzi kuwa tunakwenda kwa Waziri Magufuli.
“Moyo wangu ukapiga paah! Nikamuambia Flora, hakuamini. Tukapanda hadi ghorofa ya pili. Tulipofika, tukakaa kwenye foleni kisha tukaingia na kukutana na Waziri John Magufuli,” alisema Mbasha.
Baada ya macho yao kuamini wamekutana na waziri, Mbasha anasema aliwakaribisha chai, wakafanya mazungumzo mafupi na tangu hapo, wakashawishika kujiunga na CCM, wakawa washiriki shughuli mbalimbali za serikali pamoja na za chama hicho tawala.
“Tangu hapo, mheshimiwa alikuwa karibu sana na sisi. Akawa anatushauri njia nzuri za kupita ili tufanikiwe.
“Nakumbuka tulianza na shughuli ya uzinduzi wa Barabara ya Msamvu.
“ Tukaendelea hivyo na ikawa kila unaposikia shughuli ya uzinduzi, na sisi lazima tuwepo. Baadaye akatukutanisha na Rais Benjamin Mkapa, kisha Jakaya Kikwete, sisi tukawa kama watoto wa CCM,”alisema Mbasha.
Mwaka 2014, Mbasha na Flora waliachana baada ya Mbasha kudaiwa kumbaka shemejie kisha wanandoa hao kushutuhumiana vikali.
Mbasha alimtuhumu Flora kuhusika na ‘mpango’mchafu ili aweze kumtia hatiani mumewe, lakini hata hivyo kesi iliunguruma na hatimaye Mbasha aliachiwa huru baada ya upande wa Jamhuri kushindwa kuthibitisha mashtaka