SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumamosi, 11 Machi 2017

T media news

Kenya waomba kuwaajiri madaktari kutoka Tanzania

Serikali ya Kenya imeiomba Tanzania kuiruhusu kuajiri madaktari kutoka nchini humo ili kujaza nafasi ya madaktari walioingia kwenye mgomo kwa zaidi ya siku 90 hadi sasa.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amethibitisha kupokea ombi hilo la Serikali ya Kenya. Hata hivyo, hakutaka kutoa ufafanuzi zaidi.

“Ndio… lakini tafadhali usiniulize maswali zaidi,” Waziri Ummy anakaririwa na The Citizen.

Hivi karibuni, Serikali ya Kenya ilitangaza mpango wa kuwaajiri madaktari kutoka Tanzania, Ethiopia na Cuba kwa lengo la kuziba pengo la madaktari walioingia katika mgomo nchini humo.

Hata hivyo, Jumuiya ya Madaktari Tanzania (MAT) kupitia kwa Mwenyekiti wake mteule, Dkt. Elisha Osati jana kilieleza kuwa hakiungi mkono ombi la Serikali ya Kenya katika kipindi hiki ambacho madaktari wa nchi hiyo wako kwenye mgomo.

“MAT haiungi mkono mpango wa Serikali ya Kenya kuwaajili madaktari wa Tanzania. Labda kama ombi hili litafanyika baada ya mgomo kuisha,” Dkt. Osati aliandika kupitia mtandao wa Twitter.

Ombi hilo limekuja ikiwa ni siku chache baada ya MAT kuiomba Serikali kuwaajiri madaktari kwani kuna zaidi ya madaktari 1500 wapya waliopewa leseni lakini bado hawajaajiriwa.

Madaktari wa Kenya wameingia kwenye mgomo wakidai ongezeko la mshahara wa kima cha chini hadi shilingi milioni 9,700,000 za Tanzania, kiasi ambacho Serikali ya nchi hiyo imesema haiwezi kumudu.