SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumamosi, 11 Machi 2017

T media news

Jina la Mama Salma Kikwete Latumika Kutapeli

Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, limetoa tahadhari kwa wananchi kuhusu uwepo wa Chama cha Akiba na Mikopo (Saccos), inayotapeli watu fedha kwa kutumia majina ya watu maarufu nchini.

Tahadhari hiyo ilitolewa jijini Dar es Salaam na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Simon Sirro wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Alisema Saccos hiyo yenye jina maarufu la Focus Vicoba kwenye mitandao ya kijamii kama Facebook na tovuti inayojulikana kwa jina “http://www.vicobaloanstz. wapka-mob” www.vicobaloanstz. wapka-mob, hutumia majina ya viongozi serikalini na watu maarufu, kwa nia ya kuwatapeli wananchi.

Alisema majina ya viongozi yanayotumiwa na matapeli hao ni pamoja na jina la mke wa Rais mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Nne, Salma Kikwete, Mbunge wa Kawe Halima Mdee na Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPP, Reginald Mengi.

Aliongeza kuwa matapeli hao, hutumika kufungua akaunti za facebook na tovuti mbalimbali, ambazo hutumia kuwarubuni watu kwa kuwaaminisha kuwa wanaweza kupata mikopo yenye masharti nafuu na haraka zaidi kwa njia hiyo ya mtandao.

Alisema katika ufuatiliaji wa suala hilo, kitengo cha upelelezi wa makosa ya mtandao cha Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, kimebaini kuwa katika tovuti “http://www.vicobaloanstz. wapka-mob” www.vicobaloanstz. wapka-mob picha na jina la Mama Salma, limetumika huku kwenye ukurasa wa Facebook wakitumia jina la Mengi, likiwa ni pamoja na namba za simu 0757 308381 na 0768 199359 ambazo si za Mama Salma wala Mengi.

Aidha, alisema katika ufuatiliaji wa jambo hilo, Desema 16 mwaka jana alikamatwa mtu aliyefahamika kwa jina la Boniface Ojwando (27) baada ya kubainika kuwa anahusika katika mtandao huo wa kujipatia pesa kwa njia ya udanganyifu kupitia mitandao hiyo ya kijamii, ambapo mpaka sasa mtuhumiwa ameshafikishwa mahakamani ili kujibu mashtaka hayo yanayomkabili.

“Nitoe onyo kwa wale wote wanaondelea kufanya udanganyifu huu wa kujipatia fedha kwa njia isiyo halali kupitia mitandao ya kijamii kuacha mara moja, kwani sheria iko wazi na pindi watakapokamatwa, watachukuliwa hatua kali,”alisema Sirro.

Alitoa rai kwa wananchi wote, kutokuwa wepesi kukubali matangazo ya mikopo, yanayotolewa kwenye mitandao ya kijamii, bila kufika katika ofisi husika ili kujiridhisha kuhusu utolewaji wa mikopo hiyo, ili kuepuka kutapeliwa fedha na mali zao.