Kama unakumbukumbu nzuri basi utakuwa unakumbuka mkasa wa kijana wa ki-Afghanistan Murtaza Ahmadi aliyeingia kwenye vichwa vya habari kwenye vyombo vya habari maarufu duniani baada ya kuvaa jezi aliyoitengeneza kwa mifuko ya plastic yenye jina la mshambuliaji wa Barcelona na timu ya taifa ya Argentina Lionel Messi.
Dogo huyo ambaye anaishi Ghazni, Kusini mwa Afghanistan alitengeneza mfano wa jezi ya timu ya taifa ya Argentina na kuipa namba 10 na jina Messi.
Mkasa huo ulianzia kwenye mitandao ya kijamii na baadae harakati za kumtafuta kijana huyo kujua ni nani zikaanza mara moja hatimaye kijana akajulikana hadi mahali anapoishi.
Baada ya Messi kupata habari za kijana huyo akafanya mpango wa kukutana nae, kutokana na majukumu mengi haikuwa rahisi lakini Messi alituma jezi aliyoisaini na ikamfikia dogo na kuahidi kukutana nae atakapokuwa na nafasi.
Kama zali mwanangu, ukaandaliwa mpango wa dogo huyo kukutana na role model wake. Siku moja akasafirishwa hadi Qatar ambapo Barca walikuwa wanacheza na Al-Ahli Saudi FC na kuingia uwanjani akiwa ameshikwa mkono na Messi na badae akapata fursa ya kupiga picha na kikosi cha Barcelona.
Messi akiwa amemshika mkono kijana Murtaza (kushoto) wakiingia uwanjani
Story kama hiyo imetokea bongo Dar es Salaam baada ya kijana mmoja ambaye hajafahamika mara moja kuamua kuandika kwa wino wa kalamu jina la nyota wa Simba Ibrahim Ajib kwenye t-shirt yake iliyopauka kuonesha mahaba yake kwa staa huyo wa timu ya taifa ya Tanzania.
Ukimwangalia kwa jicho la haraka, dogo anaonekana hana uwezo wa kununua jezi ya Simba yenye jina la Ibrahim Ajib lakini bado haikuwa kikwazo kwake kuonesha ni jinsi gani anavyomzimia Ajib. Njia pekee akaona ni kuchukua kalamu yake na kuiandika mgongoni t-shirt yake jina mshambuliaji huyo wa Simba.
Huyu dogo kwa upande wangu namfananisha na Murtaza Ahmadi ambaye licha ya umasikini wa familia yake ambao ulimfanya aishie kuona jezi ya Messi ikiwa dukani lakini akaamua kuvaa mfuko wa ‘rambo’ kukidhi nafsi yake ya kuliweka jina la Messi mgongoni mwake. Lakini badae Messi alifanya ndoto za kijana huyo zikatimia.
Sasa tusubiri kuona kama Ajib atatimiza ndoto za kijana huyu mtanzania au ‘atampotezea’.