Na Yahaya Mohamed
Kama unakumbuka, juma lililopita nilikuletea sehemu ya kwanza ya makala inayomhusu kocha wa Azam FC Idd Cheche ikisimulia mambo mbalimbali kuhusu kocha huyu mzawa ambaye amepata mafanikio katika kikosi hicho baada ya kutimuliwa kwa kocha raia wa Hispania Zeben Hernandez na wasaidizi wake.
Hii ni sehemu ya pili na ya mwisho wa mwendelezo wa kile nilichokumegea kutoka sehemu ya kwanza, endelea…
Cheche anapenda kutumia mfumo upi?
Katika mambo ya mifumo haya, unaweza kupanga kutokana na nini unataka katika mchezo husika, kwa sababu unaweza ukacheza 3-5-2 lakini je, una watu wa kuwatumia katika mfumo huo?
Kila mfumo una kanuni zake, sasa ukitumia mfumo ambao huna watu wa kucheza kulingana na mfumo huo, utapata tabu. Unaweza ukaona mfumo huo haufanyi kazi lakini je, watu ulionao wanaweza kutumika kwenye mfumo wako?
Masuala ya vibali yakikaa sawa kwa kocha mpya wa Azam raia wa Romania, Cheche atakuwa msaidi wake.
Anazungumziaje ujio wa walimu wa kigeni nchini?
Kuna namna mbili unaweza ukasema, wanaweza wakaja wakaleta faida lakini vilevile wanaweza wakatuvuruga.
Kwa nini wanaweza kuleta faida, unapokwenda kwenye mji wa watu, kitu cha kwanza lazima usome mazingira ya wenyeji pamoja na kuwa umekwenda na wataalam lakini unapaswa uungane na wenyeji ujue watu wakoje na kuanza kuingiza vitu vyako taratibu.
Lakini mara nyingi wanapokuja walimu wa kigeni, basi wale walimu wa kwetu wanawekwa kando.
Pamoja na ujio huo, unadhani wazawa wanaaminiwa?
Suala hilo bado gumu sana kwa sababu kadiri unapofanya kitu, mtu analeta changamoto kwamba unabahatisha, kila mtu anasema lake.
Ni walimu gani wazawa wanamvutia Cheche?
Hilo ni swali gumu sana, unajua uanaweza kuwa unakubali baadhi ya vitu kwa mwalimu fulani baadhi ya vitu huvikubali.
Wapo walimu wa Tanzania ambao anaweza akawa mhamasishaji mzuri lakini akapungukiwa katika vitu fulani. Kwa mfano Julio, anaweza kuhamasisha kitu lakini anamapungufu yake kwa upande mwingine. Mwingine akawa mzuri katika mbinu lakini akawa na mapungufu sehemu nyingine.
Waamuzi ni kikwazo kwa Cheche ?
Hayo mambo huwa inatokea lakini hatuwezi kupata fairness kwa asilimia 100, sio rahisi lakini kama waamuzi wakijitahidi kuwa fair hasa katika baadhi ya mechi kubwa tunazocheza basi mwenye kushinda ashinde kwa uwezo wake. Isifike mahali timu ikashinda kwa mgongo wa watu fulani.
Kocha huyu anapenda au kufatilia ligi gani barani Ulaya ?
Bahati mbaya hapa Tanzania tunanyimwa haki na kulazimishwa sana kuangalia ligi ya England, lakini mimi Bundesliga inanifurahisha sana kwa sababu hata mtu akicheza na kufanya shughuli unaona kweli kazi inafanyika. Huwezi kukuta mtu mmoja anatamba muda wote na hata kama anatamba basi awe mwanaume kweli tofauti na Spain unakuta Cristiano Ronaldo na Messi siku zote wao tu.
Ronaldo na Messi je?
Kila mtu anafanya kwa namna yake na kupata kile anachokihitaji lakini nashindwa kutoa jibu, ilimradi matokeo yanapatikana.
Pamoja na Azam kushindwa kupata matokeo mazuri msimu huu, Cheche hajapoteza hata mchezo mmoja katika mechi 10 za mashindano yote alizosimama kama kocha wa timu hiyo.