Na Baraka Mbolembole
Kushindwa kupandisha timu yoyote ligi kuu Tanzania bara msimu ujao kwa Mkoa wa Dar es Salaam si pigo lakini ni dalili njema kwamba soka la Tanzania linazidi ‘kutanuka’ kila pembe ya Tanzania. Lipuli FC imerejea ligi kuu baada ya kusubiri kwa miaka takribani 15 na wamepanda mbele ya timu za Friends Rangers na Mshikamano FC za Dar es Salaam.
Singida United nayo imerejea VPL baada ya kupita takribani miaka 16 ya Mkoa huo wa katikati mwa Tanzania kushindwa kuona michezo ya ligi na huenda Njombe Mji FC ya Njombe ikaungana na timu hizo kongwe kupanda ligi kuu msimu ujao kwa mara ya kwanza ikiwa itafanikiwa kupata walau sare katika mchezo wao wa mwisho nyumbani vs Kurugenzi.
Licha ya kutokuwa na mdhamini Lipuli ilifanikiwa kutokana na juhudi, umoja na mshikamano uliokuwepo miongoni mwa viongozi wa Chama cha soka, uongozi wa klabu, serikali ya mkoa na wadau wote wa mpira ambao walihakikisha timu hiyo inapata mahitaji muhimu.
Lipuli ilipangwa kundi A pamoja na Pamba FC ya Mwanza, African Sports ya Tanga, Ashanti United, Friend Rangers, Polisi Dar FC, Mshikamano FC ( zote za Dar es Salaam) na Kiluvya United ya Pwani. Wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa sana kwa sababu ni kundi ambalo liliwafanya kusafiri mara nne kwenda Dar, mara moja Tanga na mara moja Mkoa wa Pwani.
Kuongoza kundi ambalo lilikuwa na timu Nne kutoka Dar, moja Pwani na nyingine ya Tanga si jambo rahisi kwa timu ambayo haikuwa na udhamini. Lakini wamefanikiwa kupanda na kuziacha timu hizo ligi daraja la kwanza huku Sports ikishuka hadi ligi daraja la pili.
Kundi hili awali lilionekana lingewapa nafasi nyingine mkoa wa Dar es Salaam kuongeza timu katika ligi kuu lakini wameshindwa baada ya klabu hizo kushindwa kutengeneza umoja katika klabu zao. Nakumbuka baada ya kila timu kucheza michezo mitano niliandika mahala kuwa Lipuli, Polisi Moro FC na Singida United zitapanda ligi kuu msimu ujao.
Maneno yangu yanaweza kutimia ikiwa Polisi Moro pia itafanikiwa kupanda kutokakundi B japokuwa kiuhalisia nafasi hiyo ni ngumu baada ya kuangusha pointi katika michezo miwili iliyopita. Nilisema hivyo baada ya kuona hamasa iliyokuwepo kwa wanasoka wa mikoani ambao walidhamilia na kuwekeza nguvu zao kuhakikisha timu zao zinapanda.
Kinondoni Municipal Council FC (KMC) ni timu pekee ya Dar es Salaam ambayo ilijiandaa vizuri, licha ya kwamba ilipangwa kundi gumu pamoja na timu za Mikoani timu hiyo ya Manispaa ya Kinondoni imekuwa na mwenendo mzuri na watasubiri hadi siku ya mwisho kujua hatma yao.
Mji Njombe ambayo inaongoza kundi hilo la pili kwa alama Tatu zaidi ya Polisi Moro na KMC ina nafasi kubwa zaidi ya kupanda na kunziacha daraja la kwanza timu za JKT Mlale ya Ruvuma, Coastal Union ya Tanga, KMC, Polisi Moro, Mbeya Warriors na Kurugenzi Iringa. Kumbuka tayari timu ya Kimondo FC ya Mbeya imeshushwa daraja kutoka kundi hilo la pili.
Kundi C halikuwa na timu yoyote kutoka Dar es Salaam. Kundi hilo lilikuwa na timu za Alliance School Academy ya Mwanza, JKT Mgambo ya Tanga, Mvuvumwa FC ya Kigoma, Panone FC ya Kilimanjaro, Polisi Dodoma ya Mpwapwa, Rhino Rangers ya Tabora na Singida United ambao wamepanda VPL msimu ujao kutoka kundi hilo.
Kuanzia mwanzo hadi mwishoni mwa wiki iliyopita kundi hilo lilikuwa na ushindani mkubwa baina ya timu tatu za Singida, Alliance na Rhino huku timu ya Mvuvumwa ikishuka daraja.
KWANINI DAR ES SALAAM IMESHINDWA KUPANDISHA TIMU?
Rangers na KMC angalau zilikuwa na mwelekeo wa kupanda miongoni mwa timu tano za Dar es Salaam ambazo lakini walishindwa dakika kutokana na sababu za ndani na nje ya uwanja. KMC wamekwamishwa na uzoefu huku Rangers wakianguka kwa kuamini kuwa timu yao ‘haipendwi na haitakiwi’ na baadhi ya watawala wa soka la Tanzania.
Ashanti iliangushwa na hali ya uchumi, Mshikamano walijitahidi kufanya vizuri lakini nao kama ilivyokuwa kwa KMC ilikwamishwa kwa kiasi kikubwa na uzoefu. Polisi Dar haikujiandaa kwa lengo la kupanda. Jambo zuri kwao ni kwamba hakuna timu ya Dar es Salaam iliyoteremka daraja kwenda ligi daraja la pili hivyo wanaweza kujipanga upya kwa ajili ya ligi daraja la kwanza msimu ujao.