SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumatatu, 13 Februari 2017

T media news

Kidato cha Kwanza Kupimwa Upya Uwezo,Watafanya Mtihani Mwingine wa Taifa..!!!


BARAZA la Mitihani la Taifa (Necta), linatarajia kuanza upimaji maalumu wa stadi na maarifa kwa wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza mwaka huu shule za Serikali.

Kwa mujibu wa taarifa iliyopatikana jana kutoka Necta na kusainiwa na Kaimu Mtendaji, Dk. Richard Kasuga, makatibu tawala Tanzania Bara wanajulishwa kuanza kufanikisha mchakato huo na upimaji huo unatarajiwa kuanza Februari 28, mwaka huu.

Ilifafanua kuwa wanafunzi wote waliofaulu kujiunga kidato cha kwanza mwaka huu wanatakiwa kufanyiwa mtihani maalumu kwa ajili ya kuwapima ili kubaini uwezo wao waliouonesha katika mitihani yao ya shule ya msingi.

Iliongeza kuwa lengo la kufanya hivyo ni kuwabaini wanafunzi waliofaulu kwa njia ya udanganyifu na watakaobainika wataondolewa shuleni.

“Baraza la Mitihani linawajulisha makatibu tawala kuwa litafanya upimaji maalumu wa stadi na maarifa kwa wanafunzi waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza katika shule za umma, Februari 28, mwaka huu,” ilisema taarifa hiyo.

Pia taarifa hiyo iliwataka makatibu tawala wote kuwasilisha idadi ya wanafunzi waliochaguliwa kidato cha kwanza kwa Katibu Mtendaji wa baraza hilo kabla ya Februari 10, mwaka huu.

Wakati huo huo, maofisa elimu wa shule za sekondari na wakuu wa shule za umma walitakiwa kujulishwa kuhusu mchakato huo ili kuondoa changamoto zinazoweza kujitokeza.