Msanii maarufu anayepamba video za wasanii wa muziki wa bongo Fleva (Video Queen) Agnes Gerald maarufu Masogange ameendelea kusota rumande, huku jalada lake likiendelea kuwa mikononi mwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).
Masogange (25), alikamatwa na Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kwa tuhuma za kujihusisha na uuzaji, usafirisha na kutumia dawa za kulevya.
Masogange alitarajiwa kupandishwa kizimbani Ijumaa wiki iliyopita lakini ilishindikana kutokana na majibu ya Mkemia Mkuu wa Serikali dhidi ya vipimo vyake kuonesha kama anatumia au hatumii dawa hizo kutokamilika.
Hata hivyo alitarajiwa kufikishwa tena Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu juzi ambapo alikwama tena kutokana na jalada lake kupelekwa kwa AG.
Wakili wa Masogange, Nick Kitege amesema bado jalada la Masogange lipo kwa AG na anaendelea kulifanyia kazi na pindi litakapokamilika muda wowote anaweza kupelekwa mahakamani.
Alisema jalada hilo limechelewa kutokana na taratibu za kisheria zinazofanywa ili kukamilisha uchunguzi.
“Bado tupo tunafuatilia na jalada la kesi yake kwa sasa lipo kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali pindi taratibu zitakapokamilika atafikishwa mahakamani kati ya leo au kesho.
“Kuhusu ucheleweshwaji wa kesi hiyo ni kutokana na taratibu za kisheria, hivyo Polisi waachwe wafanye kazi yao na sisi tunaangalia hatua zinazoendelea.
“Unajua hivi ni vyombo vya sheria na wanafanya kazi yao, wanahitaji muda kuchunguza na kutoa hoja zilizojitosheleza, bado wanahangaika kushughulikia suala hilo naamini leo tutapata jibu kamili,” alisema Kitege.
Julai mwaka 2013 Masogange alikamatwa Afrika Kusini katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Oliver Tambo, akiwa na mwenzake aliyejulikana kwa jina la Melisa Edward wakiwa na mzigo wa dawa za kulevya wenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 6.8.