SWALI aliloulizwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, kuhusu tuhuma zilizosambaa mitandaoni, kwamba anatumia cheti cha kidato cha nne cha mtu, zimeibua jambo jipya kuhusu tuhuma hizo.
Badala ya kujibu swali hilo, Makonda jana alitoa lugha ya vitisho na matusi kwa Mhariri wa Habari wa gazeti hili, Exuperius Kachenje, akitumia simu ya mwandishi aliyemuuliza swali hilo, Salha Mohammed.
Awali gazeti hili lilianza kufuatilia madai ya Makonda kukosa cheti cha kidato cha nne, kutokana na hatua ambazo Serikali ya Awamu ya Tano, imeshazichukua dhidi ya watumishi wa umma, wasiokuwa na vyeti hivyo ambao walishafukuzwa kazi na wako hatarini kupoteza mafao yao.
Ufuatiliaji
Katika jitihada kusaka ukweli kuhusu madai hayo, gazeti hili tangu wiki iliyopita lilizungumza na anayedaiwa kumpa cheti hicho Makonda, aliyejitambulisha kwa jina la Paul Pierre Christian.
Gazeti hili pia lilipata taarifa za ziada kutoka katika chanzo chake, zilizoeleza madai ya ukaribu wa Makonda na Christian katika maisha ya ujana wao.
Jitihada ziliendelea kutafuta taarifa sahihi, ambapo gazeti lilikuwa katika mchakato wa kupata taarifa kutoka shule ya msingi Kilomije, iliyopo wilayani Kwimba, kujua jina sahihi la kwanza alilotumia Makonda alipokuwa akisoma shuleni hapo, ambalo inadaiwa si Paul.
Kabla ya kukamilika kwa mchakato huo, ndipo gazeti lilipopata taarifa za kuwepo kwa mkutano wa waandishi wa habari ulioitishwa na Mkuu huyo wa Mkoa, kuhusu kupatikana kwa eneo la kujenga viwanda vidogo jijini humo, iliyochapishwa ukurasa wa nane wa gazeti hili.
Kutokana na umuhimu wa taarifa hizo, Kachenje alimwelekeza Salha, kutumia fursa hiyo kihabari kuzungumza pembeni na kiongozi huyo, ambapo katika hali ambayo haikutarajiwa, Makonda aliagiza simu ipigwe kwa mhariri na kutoa kauli ambazo hazikutarajiwa.
Makonda
Makonda alimuagiza Salha, kumpigia simu mtu aliyemtuma kuuliza swali hilo, ambaye ni Kachenje ili ampe jibu mtu huyo badala ya mwandishi.
Kupitia simu hiyo iliyopigwa saa 5:45 ambapo rekodi zinaonesha mazungumzo ya awali yalichukua sekunde 30, kisha akapiga tena saa 5:46 na kutumia sekunde 13, Makonda alihoji iwapo swali lililoulizwa kwake litasaidia kumtoa, Mshauri wa Kampuni za Quality Group, Yusuf Manji katika kesi inayomkabili kuhusu matumizi ya dawa za kulevya.
Aidha, Makonda alitumia simu hiyo ilipopigwa kwa mara ya pili, kumtisha mhariri huyo kwamba asisikie amemtisha mwandishi Salha.
Alipotakiwa kueleza zaidi tukio hilo, Kachenje alisema simu ya Salha ilipoingia kwake, hakuwaza jambo lolote zaidi ya kutarajia kupewa dondoo za awali za mkutano alioitisha Makonda, kwa kuwa ndio utaratibu wa kawaida wa mwandishi, kumuarifiwa mhariri kilijiri katika utafutaji habari.
“Nilisikia sauti ya Salha ikisema, huyu hapa ongea naye, nikauliza ni nani, mwandishi akajibu RC. Kusikia hivyo nikamsalimu, badala ya kujibu salamu, akanza kutoa maneno,” alisema Kachenje.
Sehemu ya mazungumzo hayo ya Makonda na Mhariri wa Habari wa gazeti hili kupitia simu ya Salha ni kama ifuatavyo:
Mhariri: “Mheshimiwa habari?”
RC Makonda: “Unadhani majibu ya swali hili yatamtoa Manji kwenye kesi ya dawa za kulevya?”
Mhariri: “Mheshimiwa, hilo linakujaje, sisi tunataka kujua kuhusu wewe?”
RC Makonda: “Nasema hivi, unadhani majibu ya swali hilo (kuhusu elimu yake) yatasaidia kumtoa Manji kwenye kesi ya dawa ya za kulevya? Huna akili wewe.” Alisema Makonda kisha akakata simu.
Hata hivyo, sekunde chache baadaye alipiga tena simu na Mhariri alipotaka ufafanuzi zaidi, Makonda alisema: “Na nisikie unamtisha au kumnyanyasa huyu mwandishi (Salha),” kisha akakata simu.
Mwandishi alivyouliza
Akisimulia alivyomfuata Makonda ili kumuuliza swali hilo baada ya kumaliza kuzungumza na waandishi wa habari Kisarawe 11 wilayani Kigamboni, Salha alisema alimuomba pembeni Mkuu huyo wa Mkoa ili amuulize swali hilo.
Kwa mujibu wa Salha, Makonda hakuwa na shaka na alikubali ombi hilo lakini baada ya kuulizwa swali hilo, Mkuu huyo wa Mkoa aliomba nafasi ili amjibu Mhariri moja kwa moja kupitia simu yake (mwandishi) na mwandishi huyo alitii. Mahojiano ya Salma na Makonda yalikuwa kama ifuatavyo;
Mwandishi: Shikamoo.
RC Makonda: Marahaba.
Mwandishi: Kuna taarifa kwenye mitandao ya kijamii kwamba unatumia cheti cha mtu cha sekondari, taarifa hizo ni kweli?
RC Makonda: Amekutuma nani?
Mwandishi: Nimetumwa na ofisi, bosi wanngu amenituma.
RC Makonda: Mpigie nimjibu.
Ndipo mwandishi akampigia Mhariri wa Habari naye alipokea simu hiyo na kutoa majibu aliyotoa.
Akizungumza tukio hilo, Salha alisema majibu ya Makonda yalimfanya ashangae kwa kuwa hakutegemea jibu alilosikia.
Katibu TEF
Akizungumza kuhusu tukio, Katibu wa Jukwaa la Wahariri (TEF), Neville Meena alisema alichofanya Makonda kinapingana na Sheria ya Huduma za Habari ya Mwaka 2016 kifungu cha 7.
“Kifungu hicho kinaeleza majukumu ya kisheria kwa mwandishi wa habari kutafuta taarifa na hilo linafanyika ili kuujulisha umma, pili ni suala la weledi.
“Kama Mkuu wa Mkoa, Makonda alifuatwa na kuulizwa kuhusu taarifa kwamba hana cheti cha kidato cha nne, ambazo zimezagaa katika mtandao, hapo alipaswa kujibu tuhuma badala ya kumshambulia Mhariri wa Habari,” alisema Meena na kuongeza:
“Makonda asitufikishe mahali vyombo vya habari vikaacha kutuma waandishi kwenye mikutano yake, itafika mahali tutawazuia na lazima niseme anakwenda kubaya. Asipambane na vyombo vya habari. Alitaja watu katika tuhuma, naye akitajwa asikilize na kujibu hoja.”
Madai mtandaoni
Mwishoni mwa wiki iliyopita kulizagaa taarifa kwenye mitandao ya jamii, zikidai kwamba Makonda anatumia cheti cha mtu cha kidato cha nne.
Taarifa hizo zilidai kuwa jina la kwanza analotumia Makonda ni la mtu mwingine anayetajwa kusoma kidato cha tano na sita katika Shule ya Wavulana Tabora, baada ya kufaulu vizuri kidato cha nne, na sasa ni mtangazaji katika redio moja ya jamii mkoani Tabora.
Katika jitihada za kupata taarifa sahihi, gazeti hili lilifanikiwa kumpata mtoa habari aliye karibu na anayedaiwa kutoa cheti cha kidato cha nne chenye ufaulu wa daraja la kwanza kwa Makonda.
Mtoa habari huyo alimtaja anayedaiwa kuwa mmiliki wa cheti anachotumia Makonda, kwa jina la Paul Cristian na kwamba Mkuu huyo wa Mkoa na mtangazaji huyo, ni marafiki wa karibu na ni kama watoto waliolelewa katika familia moja.
Kwa mujibu wa mtoa habari huyo, madai yaliyosambaa katika mtandao kwamba Makonda alipata sifuri kidato cha nne si kweli, ila alitoa taarifa zingine kutilia shaka jila la Paul, analotumia Makonda sasa. (mazungumzo mengine yamehifadhiwa).
Anayedaiwa kumiliki cheti
Gazeti hili lilifanikiwa kumpata mwandishi anayedaiwa kumpa cheti cha kidato cha nne Makonda, ambaye alijitambulisha kwa jina la Paul Christian.
“Paul Makonda nimemfahamu kupitia habari, na jina wanavyolitaja (waliotunga taarifa ya mtandaoni) wanakosea kwani mimi naitwa Paul Pierre Christian Kagezi, hatuna uhusiano, mimi Mhaya yeye Msukuma.”
Alisema watu wanaooanisha majina pasipo kufanya utafiti wa kutosha, wangeuliza kwanza kabla ya kutoa na kusambaza taarifa kwenye mitandao.
“Taarifa hizo (za kumpa cheti Makonda) si za kweli kwa sababu huwezi kutoa cheti wakati umepata daraja la kwanza kidato cha sita, utakwenda vipi chuo kikuu? Sasa niliwezaje mimi kwenda chuo kikuu halafu kwa wakati huo nimpe naye aende chuo kikuu?”Alihoji.
Cristian aliendelea kudai kuwa katika kidato cha tano na sita, alichukua mchepuo wa sayansi masomo ya Fizikia, Kemia na Hesabu (PCM), hivyo si rahisi kutoa cheti hicho kwani angeshindwa kumudu huko alikokwenda.
Alihoji kama Makonda hakufanya vema kidato cha nne au hakusoma kidato cha sita, akatumia cheti cha mtu mwingine, angeweza vipi kufanya vema katika mitihani yake ya chuo kikuu?
Alifafanua kuwa watu wamekuwa wakipika na kuoanisha majina yao, huku akiendelea kukanusha kuhusu taarifa hizo.
“Kama wanataka kumpata huyo bwanamdogo (Makonda) kwa njia hiyo wamemkosa, kwani kwa mantiki nimekuuliza ukipata daraja la kwanza kidato cha sita lazima uende chuo kikuu?” Alihoji baada ya kushindwa kujibu swali la mwandishi kuhusu chuo kikuu alichosoma na ilikuwaje akawa mwandishi wa habari.
Christian aliendelea kudai kuwa kutumia cheti kimoja kwa vyuo viwili vya Serikali, ni jambo lisilowezekana akimaanisha Makonda asingeweza kutumia cheti alichokuwa akitumia yeye.
“Sera ya Serikali ni kwamba unapata asilimia 100 ya mkopo, inakuwaje mtu huyo nimpe cheti changu wakati huo naye anakwenda chuo kikuu ambacho nacho ni cha Serikali?” Aliendelea kuhoji.
“Huyo bwana anajitegemea yeye kama yeye, na walichokifanya wao (waliosambaza taarifa mtandaoni) kwa makusudi yao bila shaka wana lengo lao, wao wametaka kuingiza hoja ambazo hazina mashiko.
“Cheti cha daraja la kwanza unauza kwa gharama gani? Nimesoma shule ya msingi na sekondari, (Makonda) alikuwa na fedha kiasi gani za kunipa ili nimuachie cheti? Inaweza kukuingia akilini kweli?”Alihoji Christian.
Alidai hata namba ya Makonda hana, huku akibainisha kutokumbuka namba za shule alikomaliza kidato cha nne pamoja na za cheti chake cha kidato cha nne.