Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, jana iligeuka kuwa uwanja wa masumbwi, baada ya wafuasi wa Chama cha Wananchi (CUF) kupigana na kusababisha watu watatu kujeruhiwa.
Wafuasi hao ni wa Bodi ya Wadhamini ya Chama walio upande wa Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad na wanaomuunga mkono Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba.
Tukio hilo la aina yake, lilitokea kabla ya kuingia kwenye chumba cha mahakama, tayari kwa kusikiliza uamuzi wa kujitoa au kuendelea kwa Jaji Sekiet Kihiyo kusikiliza kesi hiyo na baada ya kutoka mahakamani.
Hata hivyo, Jaji Kihiyo alitupilia mbali maombi ya bodi ya wadhamini kwamba asiendelee na kesi hiyo, kwa madai kwamba hawana imani naye, kwa kusema kuwa maombi hayo, hayana msingi kwa kuwa sheria inamruhusu kutojitoa kirahisi kwenye kesi.
Alieleza kuwa wadau hawana nafasi kujichagulia jaji wanayemtaka. Kabla ya kuingia kwenye chumba cha mahakama, mfuasi mmoja wa Profesa Lipumba na wanaodaiwa kuwa wafuasi wa Maalim Seif, walianza kurushiana ngumi na kuleta mtafaruku katika eneo la watu wanaosubiria kesi zao kuitwa huku Lipumba akionekana kulindwa na walinzi mbalimbali.
Aidha, baada ya jaji kutoa uamuzi huo, wafuasi wote walitoka nje, ambapo wakati Profesa Lipumba akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kesi hiyo, wafuasi hao walianza kupigana na kujeruhi watu watatu, ambapo mmoja wao, aliyejulikana kwa jina la Robert Samson, alijeruhiwa kwa kutumia kitu chenye ncha kali shingoni na kusababisha kuvuja damu nyingi.
Hali hiyo iliendelea kwa wafuasi wa bodi ya udhamini, kulalamikia walinzi wa mahakama, kwamba ni kwa nini wanakagua watu, lakini wameshindwa kuwaona wenye silaha, ikiwemo visu na kusababisha watu wao kujeruhiwa.
Pia walidai kuwa licha ya kuwepo kwa askari wengi mahakamani hapo wakiwa na silaha, walishindwa kutuliza ghasia hiyo, ambayo imeleta madhara, kwa kuwa kila mfuasi aliyemuona adui yake alishikana naye shati na kupigana.
Kabla ya vurugu hizo kuisha, Profesa Lipumba na wafuasi wake walipanda magari yao huku wakimwimbia nyimbo za kumsifu mwenyekiti huyo na kuondoka. Waliwaacha wafuasi wa bodi ya wadhamini, wakilalamikia kitendo cha kupigwa.
Walijiapiza kwamba watajipanga ili siku kesi hiyo itakapoitwa tena, watahakikisha wanawadhibiti wapinzani wao na kwamba wataleta madhara makubwa mahakamani hapo.
Awali, akitoa uamuzi huo, Jaji Kihiyo alisema kuwa Novemba 10 mwaka huu, mawakili wa bodi ya wadhamini ya CUF, wakiwakilishwa na Rahim Khalfan, waliandika barua kwa Msajili wa mahakama hiyo, kuomba jaji huyo ajitoe, kwa kuwa wateja wao hawana imani naye.
Alisema kuwa hawezi kujitoa, kwa sababu zisizo za msingi, kwamba anaupa upendeleo upande wa washitakiwa na kuwaacha waombaji wakati hakukuwa na mazingira ya kuruhusu kutolewa hoja kwa pande zote.
“Mahakama ya Rufaa inasema majaji au mahakimu hawatakiwi kujitoa kwa urahisi kwenye kesi. Pia sheria hairuhusu wadau ambao wanakuja kwa mara ya kwanza mahakamani na hawajui taratibu za mahakama watake kujichagulia jaji,” alisema Jaji Kihiyo.
Alisisitiza kuwa jaji au hakimu ana mamlaka chini ya sheria, kujitoa au kuendelea kusikiliza shauri, kama ataridhika kwamba sababu zilizotolewa, zina nguvu ya kushawishi afanye hivyo.