SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumanne, 27 Desemba 2016

T media news

SIMULIZI FUPI: ‘UMENIUA ASHURA’


Ashura .. oooohh.. Ashura … umeniua!!!
Kwa nini umenifanyia hivi Ashura…??? Nilikukabidhi moyo wangu nikiamini kuwa unanipenda. Ndiyo, niliamini hivyo tangu siku ile ya kwanza tulipokutana pale TILDO mwaka 2010, wakati tunarejesha fomu zetu za maombi ya mkopo kwenye ofisi za bodi ya mikopo ya elimu ya juu.

Naikumbuka sana siku hiyo… ulikuwa umevaa baibui la rangi nyeusi, vazi lililoyasitiri maungo yako na kukufanya uonekane mwanamke mwenye staha, nikapendezwa na wewe na Moyoni nikafikiria kukufanya uwe mke, tabibu wangu wa moyo.
Wakati bado napiga hesabu za kukufuata … mara ghafla nikakuona ukichapua hatua kuja mahali nilipo. Sikuwa na uhakika kama ulikuwa unakuja kwangu mpaka ulipofika mbele yangu na kunisalimu, “Kaka mambo?”
Siyo siri Ashura… sauti yako iliufanya moyo wangu kuzizima mara tu ilipotua masikioni kwangu. Sauti yako ilikuongezea alama na kukufanya uwe mrembo maradufu, na mara shauku ya kuwa nawe kama mke ikakita barabara kwenye kitako cha moyo wangu.
Kwa kuwa sikutaka kuonekana dhaifu kwa viumbe wa jinsia yako, nilijikaza kiume na kuitikia “powa, inakuwaje?” nilitoa sauti kavu, japo moyoni nililainika kama siagi kwenye kikaango cha moto.
Baada ya salamu ulinieleza shida yako nilikuelewa, tukatoka nje, tukavuka barabara mpaka upande wa pili kwa yule mwanasheria aliyekuwa akitia sahihi na kugonga muhuri kwenye sehemu ya kiapo cha wakili, sehemu ambayo ilikuwa tupu kwenye fomu yako kabla hatujafika kwa yule mwanasheria!
Baada ya kutoka kwa Yule mwanasheria tulivuka barabara na kurejea tena TILDO, ukakusanya fomu yako. Huo ukawa wasaa wa sisi kufahamiana, wasaa ambao baadaye ulituweka kwenye dunia ya mapenzi…mapenzi mazito!
Tukawa kama jozi ya viatu visivyofanana ila vyenye kurandana, naweza kusema tulikuwa kama mapacha wa hiyari tuliokulia na kuzaliwa kutoka katika matumbo tofauti. Kwa ufupi tuliendana sana.
Tukapanga mengi juu ya maisha yetu ya baadaye, ikiwemo kufunga ndoa licha ya tofauti za kidini zilizokuwepo baina yetu…mpaka hapo naweza kusema; ‘kweli mapenzi ni upofu!’
Siku zikaenda….zikaenda hatimaye ukafika wakati tukayaanza masomo yetu ya elimu ya juu. Wakati wewe ukiwa ‘DUCE’ Chang’ombe mimi nilikuwa ‘MUCE’ Iringa, wote tukisoma shahada ya kwanza ya ualimu.
Umbali kwetu haukuwa kikwazo cha mapenzi yetu, tukaendelea kuwasiliana kwa simu tukijuliana hali na kutiana moyo katika masomo yetu, huku mipango yetu ikiwa palepale kwamba siku moja tufunge ndoa tuishi kama mke na mume..
Katika mazungumzo yetu hayo, mara swali likaibuka, “Tutafunga ndoa ya namna gani ilhali twapishana kwa imani ya dini?”
Nilikusihi ubadiri dini ili tufunge ndoa kanisani, ukalipinga suala hilo kwa sababu ambazo hata mimi niliziafiki. Ulidai kuwa wewe ni yatima ambaye umelelewa na babu na bibi, na ukazidi kudai kuwa babu yako ni kiongozi mkubwa wa kidini, hivyo wewe kubadiri dini ni sawa na kuifungua milango ya laana kutoka kwa babuyo, halikadhalika pia utengano baina yako na nduguzo, nilikuelewa na nikakukubalia kwa sababu siku zote nilitaka uwe mwenye furaha, na katu sikutaka kukuona mwenye huzuni tangu machoni mpaka moyoni. 
Kwa sababu ya kukupenda sana, upendo usio kifani nilifikiria na kujishauri sana hatimaye nikaamua kubadiri dini kwa ajili yako, nikaitwa Mustafa baada ya miaka mingi ya kuitwa John…jina nililopewa na wazazi wangu muda mfupi baada ya kuzaliwa.
Ulifurahi sana, jambo ambalo lilinipa faraja kwa kuwa nilitaka kukuona mwenye furaha!
Mwaka wa kwanza wa masomo ukaisha, tukaingia wa pili bila misukosuko kwenye masomo yetu. Muda wote huu ulipita nikiwa siijui hata tupu yako, achilia mbali kukubusu jambo ambalo sijawahi hata kuthubutu baada ya wewe kuniambia kuwa; “Ni dhambi kuikaribia zinaa” hapo nilikuelewa kwa sababu hata mimi nalijua andiko hilo mujarab.
Kwa kuwa mimi ni mwanaume rijali, nilikusihi tuitafute ‘NUSRA’ ili kujiepusha na dhambi ya kuzini, dhambi ambayo ilikuwa ikitukaribia siku hadi siku.
Ashura mpenzi wangu ukanipinga kwa kusema haitawezekana kwa sababu ‘Mshika mbili moja humponyoka’ hivyo tusubiri mpaka pale tutakapomaliza shule. Nilikuelewa na nikazidi kumuomba Alah anijaalie moyo wa subira.
Kwa kuwa Alah si mnyimi wa fadhila, alinijaalia subira mpaka mwaka wa tatu wa masomo yetu ulipoisha. Tukahitimu salama salmin tena kwa ufaulu wa alama za juu. Ashukuriwe Jalali!
Baada ya shule kweli tulifunga ndoa, ndoa ambayo ilinifanya niyagundue mengi kwenye mwili wako. Kwanza; Ashura ulinidanganya kuwa wewe ni ‘bikra’, kumbe si kweli na nilipokuuliza ulidai kuwa; labda ilitoka yenyewe baada ya wewe kuendesha baiskeli kwa umbali mrefu ulipokuwa ukienda kuteka maji kisimani, na ulipoenda kusaga kwenye mashine ambayo ilikuwa kijiji cha pili kutoka kijijni kwenu. Na kwa hili pia nilikuelewa!
Naweza kusema wewe ni mwenye bahati Ashura, ndiyo wewe ni mwenye bahati kwa sababu umejaaliwa mume ambaye ni muelewa na mvumilivu…lakini kwa makusudi kabisa umeamua kuniua!
Kwa nini Ashura…kwa nini….umeniambukiza ukimwi? Wakati unajua fika kuwa mimi ndiye mtoto wa pekee kwa yule mama mjane ambaye alijitoa kwa hali na mali kuhakikisha mwanaye nasoma kwa karo iliyotokana na biashara ya ubwabwa!
Eti unanituliza kwa kuniambia, “I’m sory!” I’m sory ina maana gani baada ya kunichafulia damu kwa virusi?
Mwanamke niliyekupenda, nikakuamini, nikakukabidhi moyo wangu….leo umeniua!! Umeniua Ashura…umeniuaa!!!

MWISHO

toa maoni yako