ASKOFU Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Eusebius Nzigilwa, amesema kanisa halijabariki utoaji mimba na wakristo waliowahi kufanya hivyo wanapaswa kutubu.
ASKOFU, MHASHAMU EUSEBIUS NZIGILWA.
Akihubiri katika misa ya Krismasi iliyofanyika kwenye Kanisa Kuu la Mtakatifu Joseph jijini Dar es Salaam jana, ikiwa ni kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo karibu miaka 2000 iliyopita, alisema zipo nchi za Ulaya na Afrika kwa sasa zimebariki utoaji mimba kuonekana ni jambo la kawaida.
Alisema kuishi ndani ya tumbo la mwanamke na kuzaliwa kwa Kristo ni uthibitisho wa uhai ambao mwanadamu hana mamlaka nao.
“Baadhi ya mataifa kama Ulaya, Marekani na sasa inaingia Afrika, mwanamke ana uhuru wa kuzaa au kutoa mimba, ni kinyume cha mpango wa Mungu. Kristo katuthibitishia kuwa uhai unaanzia tumboni mwa mama halafu anakuja mwanadamu mmoja anamuambia ruksa kutoa mimba,” alisema.
Askofu Nzigilwa alisema Wakristo hawapaswi kufanya hivyo huku akisisitiza: “Waliowahi kupata mimba na kuitoa waende wakaungame dhambi hiyo. Msikubali kuingia kwenye propaganda ya aina hiyo.”
Alisema Yesu ni mwanga, hivyo atumike kuwatoa watu kwenye giza, na kwamba matatizo yanapozidi, linaonekana giza ni hatari kwa kuwa mtu anaweza kuyumba na kupelekwa kokote.
“Tunaliondoa giza kwa kukaribisha nuru, imekuja ulimwenguni ila watu wanakimbilia giza. Ni wakati wa kuamka na kutoka gizani kwa kutenda matendo ya amani na kuuchukia uovu,” alisema na kuongeza:
“Tunaishi katika ulimwengu ambako watu wanapenda giza kuliko nuru, tusiyakubali hayo maisha.”
Alisema shinikizo la utoaji mimba limepenyezwa Afrika huku kukiwa na masharti magumu, jambo ambalo halipaswi kukubalika kwa Watanzania wenye kumjua Mungu.
“Baba Mtakatifu ametoa kibali kwa wale ambao walitoa mimba kwa sababu mbalimbali kama kutengwa na jamii, ofisi, familia kiasi cha kushindwa kuishi.
Lakini pamoja na yote, lazima kanisa likwambie umetenda dhambi, unapaswa kuungama kwa mujibu wa taratibu,” alisisitiza.