SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumanne, 15 Novemba 2016

T media news

Wanafunzi wakumbwa na ugonjwa wa kuanguka

Wanafunzi wa kike 12 wanaosoma Shule ya Msingi Nditi, Wilaya ya Nachingwea, mkoani Lindi, wamekumbwa na ugonjwa wa kuanguka ghafla na wengine kupoteza fahamu, walipokuwa wakicheza katika viwanja vya shule hiyo.

Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Amon Livigha, alikiri kutokea tukio hilo katikati ya wiki iliyopita, saa mbili asubuhi.

Alisema baada ya tukio hilo, baadhi ya wazazi walifika shuleni hapo na kuwachukua watoto wao na kwenda nao nyumbani.

“Nilipata taarifa ya kuanguka kwa wanafunzi hao nikiwa darasani nafundisha, hivyo kutokana na uzito wa tatizo, nililazimika kukatisha masomo na kwenda kuwahudumia watoto hao.

“Wakati tukiendelea kufanya utaratibu wa kuwakimbiza wanafunzi hao kituo cha afya kupatiwa huduma, baadhi ya wazazi walikataa watoto wao wasipelekwe hospitali na kuondoka nao,” alisema.

Mwalimu Livigha alisema kutokana na tukio hilo, kamati ya shule, wazazi na uongozi wa Serikali ya kijiji na kata hiyo wamekutana kujadili suala hilo.

Mtendaji wa kata hiyo, Juma Mng’anga, alikiri kutokea tukio hilo na kueleza kuwa tayari wameshatoa taarifa makao makuu ya wilaya, Nachingwea.