Na Baraka Mbolembole
KOCHA mkuu wa Mbeya City FC, Mmalawi, Kinnah Phiri amenukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari akisema timu yake itaachana na golikipa, Juma Kaseja baada ya kumaliza mzunguko wa kwanza wa ligi kuu Tanzania Bara bila huduma ya kipa huyo wa zamani wa Moro United, Simba SC, Yanga na timu ya Taifa ya Tanzania.
City inayocheza VPL msimu wa nne mfululizo tangu walipopanda kutoka ligi daraja la kwanza mwaka 2013 imemaliza michezo 15 ya mzunguko wa kwanza msimu huu wakiwa katika nafasi ya 8 na pointi 19.
Wamefanikiwa kushinda game tano, sare nne na kupoteza michezo sita.
Nilimtafuta msemaji wa timu hiyo, Dismas Ten na kumuulizia kama watafanya usajili na kupunguza wachezaji wakati huu wa usajili wa dirisha dogo.
“Bado hatujatoa taarifa rasmi, lakini natumaini wiki ijayo kutakuwa na taarifa mpya. Ningeomba tuvute subira kidogo kwa sasa hakuna kinachoendelea.” anasema Ten.
“Kuhusu kuongeza wachezaji wapya na kupunguza wengine, hilo ni lazima ndiyo maana nikasema ntakuwa na taarifa nzuri wiki ijayo kwa sababu taarifa (ripoti) ya mwalimu bado inapitiwa.
“Kumekuwa na taarifa katika mitandao ya kijamii kuwa Simba SC inafukuzia saini ya kipa namba moja wa City raia wa Malawi, Owen Chaima.
“Hakuna shida, kama Simba wanamuhitaji golikipa wetu, tunaweza kuwapa, muhimu wafuate taratibu tu. Waje mezani tukubaliane.” amesema Ten.
Wakati huo huo mkuu huyo wa kitengo cha habari klabuni hapo amethibitisha kuanza safari ya kutoka Mbeya kuelekea Dar es Salaam kwa kikosi chao cha pili kwa ajili ya michezo ya ligi kuu ya vijana.
“Timu yetu ya U20 imeagwa rasmi leo Jumanne na kuanza safari ya kuelekea jijini Dar tayari kwa michezo ligi kuu ya vijana. Vijana 20 na viongozi watatu watakuwa wapo katika msafara huo.”