Kitendo cha Rais John Magufuli kukataa mialiko 44 kati ya 47 ya nje ya nchi kimeokoa zaidi ya Sh5 bilioni na baadhi ya wasomi waliohojiwa kuhusu hatua hii wametofautiana. Wapo waliopongeza na wengine wakisema kusafiri kuna umuhimu mkubwa kwa Taifa.
Novemba 4, katika mahojiano na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari, Rais Magufuli aliwaambia kuwa mwaka huu alipata mialiko 47 ya kusafiri nje ya nchi lakini aliamua kwenda mitatu.
Kwa mujibu wa makadirio yaliyofanywa na gazeti hili, Rais Magufuli ambaye amekuwa akisisitiza kuhusu kubana matumizi amefanikiwa kuokoa Sh5.7 bilioni.
Kiasi hicho cha fedha ni makadirio ya wastani wa fedha ambazo Rais Magufuli na msafara wa watu 50 ambao angeongozana nao wangetumia kwenye safari hizo 44 kwa siku tatu kila safari.
Katika fedha hizo, kwa makadirio ya wastani ya posho anayotakiwa kulipwa mtumishi wa Serikali anaposafiri nje nchi ni dola za Marekani 400 sawa na Sh872,000 kwa siku.
Hivyo endapo Rais Magufuli angesafiri nje ya nchi na wajumbe 50 kwa siku moja, wajumbe hao wangelipwa jumla ya Sh43,600,000.
Iwapo safari hiyo ingekuwa ya siku tatu, wajumbe hao 50 wangelipwa posho jumla ya Sh130,800,000.
Kiasi hicho cha fedha kikizidishwa kwa mialiko ya safari 44 ambazo Rais Magufuli hakwenda huenda akawa ameokoa Sh5.7 bilioni.
Taarifa ambazo gazeti limezipata kutoka katika vyanzo vya kuaminika zinaeleza kuwa kuna madaraja mawili ya malipo ya posho kwa watumishi wa Serikali wanaposafiri nje ya nchi.
Madaraja hayo ni A na B. Kwa mujibu wa vyanzo hivyo, malipo ya posho kwa safari katika nchi za Bara la Ulaya na Amerika ambayo ni daraja A ni dola za Marekani 420 sawa na Sh915,600.
Malipo ya posho kwa safari za nchi za Bara la Asia na Afrika ambayo ni daraja B ni dola za Marekani 380 sawa na Sh828,400.
Vyanzo hivyo vimeongeza kuwa kuna mahitaji matano ambayo mtumishi anatimiziwa anaposafiri kwenda nchi ya nje ambayo ni fedha za suti, fedha za kujikimu na usafiri wa ndani atakapokuwa katika nchi husika. Pia, mtumishi anapewa ‘poketi money’ sanjari na kuongezewa posho endapo safari yake itazidi saa nane akiwa angani.
Mtazamo wa wadau
Akizungumzia hatua hiyo ya Rais Magufuli, Profesa wa uchumi, Chuo Kikuu cha Mzumbe, Honest Ngowi alisema kwa diplomasia ya uchumi hivi sasa, ni afya Rais kutoka kwenda nje hasa ikiwa safari hizo zitakuwa za mkakati kwa manufaa ya Taifa.
“Sijajua mialiko aliyotakiwa kwenda na akaikataa, lakini ni muhimu Rais akasafiri kwenda nje kujifunza na kubadilisha mawazo kama tunavyowapokea viongozi wengine hapa nchini,” alisema Profesa Ngowi.
Hata hivyo, Profesa Ngowi alisema hana taarifa za kiundani za aina ya mialiko aliyoikataa Rais Magufuli ili atoe maoni yake ya faida na hasara kwa kiongozi huyo wa nchi kukubali michache na kukataa mingi.
Profesa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Benson Bana alisema safari za nje ya nchi si vipaumbele vya Rais Magufuli na kwamba ameamua kubaki nchini huku akiwakilishwa na viongozi walio chini yake ili kupunguza gharama.
“Huo ni uamuzi mzuri na ningemshangaa Dk Magufuli kama anawakataza viongozi walio chini yake wasisafiri nje ya nchi halafu yeye akawa anasafiri kila wakati,” alisema.
Alisema wa Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete alisafiri sana kwenda katika nchi mbalimbali ambako huko aliweka mtandao imara wa kidiplomasia.
“Sasa Magufuli akaona yeye aelekeze nguvu kufanya kazi za ndani ya nchi,” alisema.
Alisema hata nchi ambazo amezitembelea kama Rwanda ni kwa sababu kulikuwa na umuhimu wa kwenda yeye mwenyewe.
“Unakumbuka Rwanda walikuwa watumiaji wakubwa wa Bandari ya Dar es Salaam na walianza kujiondoa taratibu, katika mazingira kama hayo unatakiwa kwenda mwenyewe bila kuwakilishwa,” alisema.
Alisema hakuna umuhimu kwa Rais kwenda kwenye mikutano na badala yake aendelee kuwakilishwa na viongozi walio chini yake ili kupunguza gharama.
“Nampongeza kwa kuwa ameanza vizuri, ameenda Kenya na Uganda kwa kuwa wao ni majirani ambao ni wadau wakubwa katika diplomasia ya kiuchumi,” alisema.
Profesa wa Chuo Kikuu Katoliki Ruaha mkoani Iringa (Rucu), Gaudence Mpangala alisema kuna umuhimu kwa Rais kufanya ziara za nje ya nchi anakoalikwa na kuhudhuria mikutano mbalimbali ya kimataifa.
Alisema licha ya kuwa ziara za Rais huwa ni zenye gharama kubwa, lakini kuna umuhimu wa yeye mwenyewe kwenda huko badala ya kuwakilishwa na vingozi wengine.
Alisema: “Unapokutana na marais wenzako kuna umuhimu katika medani za kiuchumi kwa kuwa unakuwa na mamlaka ya kuzungumza kila jambo linalohusiana na nchi yako badala ya mtu anayekuwakilisha ambaye mambo mengine hawezi kuyajibu hadi apewe ruksa.”
Alisema tusifikirie gharama anazotumia na ujumbe wake kwenda nje ya nchi badala yake tufikirie pia faida zinazotokana na Rais mwenyewe kwenda nje ya nchi.
chanzo gazeti la mwananchi