Na Athumani Adam
Siku ya Jumapili iliyopita timu ya taifa ya mpira miguu ya Tanzania, Taifa Stars ilikuwa kule nchini Zimbabwe kucheza mechi ya kirafiki dhidi ya timu ya taifa ya nchi hiyo. Zimbabwe wakiwa kwenye kiwango bora wakaichakaza Stars kwa ushindi wa mabao 3-0 kwenye uwanja wa taifa pale jijini Harare.
Kwenye orodha ya wachezaji ishirini na tatu wa Zimbabwe walioitwa na kocha Calisto Paswa ambaye aliwahi kuwa nyota wa zamani wa timu ya Dyanamos pamoja na timu ya taifa lilikuwepo jina la beki wa Azam FC ya hapa nchini, Bruce Kangwa.
Ukiondoa Kangwa, hakuna mchezaji mwingine yeyote raia wa Zimbabwe kutoka Tanzania aliyeitwa na Calisto Paswa. Si Dionald Ngoma, Thaban Kamusoko wala Method Mwanjali ambao wote ni wachezaji nyota kutoka Zimbabwe wanaotesa kwenye VPL wakiwa na vilabu vya Simba na Yanga.
Sidhani kama Mwanjali, Kamusoko pamoja na Ngoma kama wangekuwa raia wa Tanzania kwa kipindi hiki wangekosa kwenye kikosi cha Stars. Lakini wanakosekana kwenye timu yao ya taifa sababu ya kuzidiwa uzoefu (exposure) na wachezaji wanaocheza kwenye ligi kubwa kama PSL ya nchini Afrika Kusini
Kikosi cha Zimbabwe kiliundwa na wachezaji wanaocheza ligi ya ndani, PSL ya Bondeni pamoja na nje ya Afrika. Huu ndio uzuri wa kuwa na ligi nzuri ya ndani pamoja na professionals wa kutosha nje ya nchi.
Zimbabwe wana professionals wengi tu wa kutosha, ndio maana Calisto Paswa alikuwa na jeuri ya kuwaacha kina Mwanjali ambao wamecheza zaidi ya asilimia tisini ya mechi wakiwa na vilabu vyao vya Simba na Yanga.
Mlinzi kama Bruce kangwa wa Azam angeitwa vipi kwenye timu ya taifa kama Costa Nhamoinesu anayecheza kwenye klabu ya Sparta Praha ya Jamuhuri ya Czech asingekuwa na majeruhi?
Kumbuka Kangwa na Costa wote wanacheza nafasi moja upande wa beki ya kushoto hata kwenye taarifa iliyotolewa na kocha wa Zimbabwe kupitia mtandano wa chama cha soka nchini alisikitishwa kwa kumkosa Costa Nhamoinesu. Pia akasikitishwa kwa kumkosa professional mwwingine Macanley Bonne anayecheza ligi daraja la pili nchini Uingereza kwenye klabu ya Colchester United
Bonne alizaliwa kule Ipswich nchini England na wazazi wenye asili ya Zimbabwe, hivyo bado anaonekana kuwa na utata kuichezea timu ya taifa ya Zimbabwe. Paswa kwanini amlilie mchezaji wa ligi daraja la pili Uingereza? Jibu ni jepesi tu ushindani wa daraja la pili England ni mkubwa zaidi kuliko ligi ya Zimbabwe.
Pia kwenye nafasi hiyohiyo kuna mlinzi ambaye bado hajachagua taifa la kuchezea kati ya Zimbabwe auEngland, anaitwa Tendayi Darikwa kutoa Burnley ya England.
Zimbabwe wamefanikiwa kufuzu kwa AFCON ya tatu mapema mwezi Januray mwaka ujao kupitia nyota wake waliosambaa nje ya mipaka ya Zimbabwe. Acha Paswa awe jeuri kuwaacha kina Kamusoko ambao sisi tunawatamani.
Haikuwa ajabu kuona Stars ikipoteza kwa staili ile pale Harare. Ni ngumu kupambana kupitia professionals watatu tu waliopo kwenye safu ya ushambuliaji pekee, yaani Samatta, Maguli na Ulimwengu, kwenye safu ya kiungo na ulinzi hakukuwa na professional hata mmoja.
Kikosi chetu kinaundwa na wachezaji wengi kichupikizi ambao wanahitaji kwenda kukomaa kwenye nchini za ushindani. Bahati mbaya hili la kutoka kwenda nje limekuwa ni kitendaliwi cha muda mrefu kilichokosa ufumbuzi.