MWENYEKITI wa Mtaa wa Mwangaza katika Halmashauri ya Mji Tarime kupitia Chadema, Abdalah Ismail Maindi, amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Tarime akituhumiwa kupokea rushwa ya Sh. 11,000 kutoka kwa mwananchi aliyefahamika kwa jina Magara Magembe Masatu.
Inadaiwa kuwa Masatu alitaka kusainiwa na kugongewa mhuri katika fomu zake za kitambulisho cha taifa.
Akisomewa shitaka hilo jana Novemba 16 katika kesi ya jinai namba 938/2016 mbele ya Hakimu wa Mahakama ya Wilaya Tarime, Amoni Kahimba, Mwanasheria wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Martine Makani, alidai kuwa Novemba 15 saa 9 mchana katika Ofisi ya mtendaji wa Kata ya Nyamisangura mjini Tarime, Maindi alimuomba Masatu Sh. 11,000 alipofika ofisini kwake kupata huduma ya kusainiwa na kugongewa mhuri katika fomu zake za kuomba kitambulisho cha taifa.
Kamani alidai kuwa Maindi alidai fedha hizo ndipo asaini na kugonga mhuri na kuwa licha ya Masatu kuomba msaada huo, mwenyekiti aligoma kusaini na kugonga muhuri hadi fedha hizo zitolewe.
Makani alidai kuwa Masatu baada ya kukosa huduma alikwenda ofisi za Takukuru na kutoa taarifa ndipo alipopewa fedha hizo na kuandaa mtego uliofanikisha kukamatwa kwa Maindi baada ya kuzipokea fedha hizo ambazo hazikuwa na stakabadhi yoyote.
Hata hivyo, mshitakiwa alikana shitaka hilo huku akidai kuwa ni michango waliojiwekea katika kata yao ya kufanikisha ujenzi wa madarasa na kuomba apewe dhamana.
Wadhamini wawili walijitokeza na kumdhaminiwa kila mmoja kwa kusaini bindi ya Sh. milioni nne. Kesi hiyo itatajwa tena Desemba Mosi, mwaka huu.
Source: Nipashe