Barcelona wametangaza kupata dili jipya la udhamini wa miaka minne kutoka kampuni ya Biashara ya Kijapani ya Rakuten ambayo itachukua nafasi ya Qatar Airways kama mdhamini wa jezi kuanzia msimu ujao.
Dili hilo linatajwa kuwa na thamani ya euro mil 61 kwa msimu kama klabu hiyo inashinda taji la La Liga na Champions League, dili ambalo litazidi lile ya Manchester United la Chevrolet lenye thamani ya paundi mil 52 kwa msimu. Mkataba wa Man United ulikuwa na thamani kubwa zaidi Ulaya nzima msimu uliopita, huku ule wa Barca na Qatar Airways ulikuwa na thamani ya euro mil 33.
Rakuten ni kampuni kubwa la kibiashara lililopo jijini Tokyo Japan na ni miongoni mwa makampuni makubwa ulimwenguni yanaoongoza kwa mauzo. Mtendaji Mkuu wake Hiroshi Mikitani ambaye alikuwepo jana wakati dili hilo likitangazwa alianzisha kampuni hiyo mwaka 1997 na sasa linakadiriwa kuwa na zaidi ya wateja mil 18 duniani.
Rais wa Barcelona Josep Maria Bartomeu alifafanua kwamba mazungumzo ya awali yalifanywa na Gerard Pique, ambaye aliandaa chakula la usiku pamoja na Mikitani huko San Francisco msimu uliopita.
“Hatukuwa na haraka kutafuta mdhamini msimu uliopita kwasababu tulitaka kufikia makubaliano yenye maslahi,” Bartomeu alifafanua wakati akifanya presentation.
“Haya ni makubaliano ambayo yanahusisha kampuni kubwa duniani lenye uzoefu mkubwa ambalo linaweza kuchangia mafanikio makubwa kwa klabu. Tunaamini ushirikiano kati ya pande hizi mbili utachagiza mafanikio makubwa katika nyanja za kibiashara na kimichezo. Hii ilianza mwaka 2015 wakati Pique alipoandaa chakula cha usiku huko San Francisco wakati klabu ikiwa ziarani nchini Marekani.
“Gerard na mke wake Shakira ni marafiki wa karibu sana wa M Mikitani. Ametusaidia sana kukutana na Mikitani, hivyo tunamshukuru sana.”