Na Baraka Mbolembole
SIMBA SC wanajinasibu ya kwamba wataifunga Yanga SC katika mchezo wa raundi ya kwanza Ligi kuu Tanzania Bara siku ya Jumamosi ijayo.
Wanajivunia safu yao ya ulinzi, wana tambia ubora wa timu yao katikati ya uwanja, huku wakiamini safu ya mashambulizi ya Shiza Kichuya, Laudit Mavugo na Ibrahim Ajib inaweza kufunga katika mechi yoyote ile.
Wapo katika ‘umbo bora’ kimchezo lakini niwakumbushe tu wanakwenda kukabiliana na timu ‘timamu kimwili na kiakili’ na yenye ubora wa hali ya juu kuliko wao. Yanga ni bora zaidi ya Simba, huo ndio ukweli uliopo na Simba inajaribu kujiweka sawa baada ya ‘msoto’ wa miaka minne iliyokwisha bila mafanikio.
Ubora wa Yanga hauwezi kupimwa kwa kiwango chao cha chini walichokionesha katika game waliyopoteza ndani ya uwanja vs Stand United wikendi iliyopita. Kuanzia namba moja hadi mchezaji wa 11, Yanga wako vizuri.
Wana safu imara ya ulinzi, wana viungo makini na safu ya mashambulizi yenye makali katika ufungaji ambayo tayari ilishawaumiza katika michezo miwili ya mwisho waliyokutana.
Kiufundi, Simba wana mapungufu mengi licha ya kwamba wamefanikiwa kushinda michezo mitano na kutoa sare mara moja katika game zao Sita msimu huu.
Udhaifu wao mkubwa ni katika nafasi ya golikipa ambayo ni wazi raia wa Ivory Coasta, Vicent Anghban ataanza. Kipa huyo aliruhusu magoli manne katika mipambano miwili waliyokutana msimu uliopita. Anapendelea sana kucheza nje ya lango lake huku mipira ya krosi ikiwa ni tatizo kubwa kwake.
Yanga ni timu inayotegemea mipira ya krosi, kona na faulo kumaliza mchezo kutokana na aina ya washambuliaji wao walionao kikosini. Si hivyo tu, safu ya kiungo ya Simba hupendelea kucheza mchezo wa pasi fupi fupi huku wakiwa si wazuri katika upigaji wa pasi.
Pasi zao nyingi hazina nguvu, hazina kasi na jambo hilo litakuwa na faida kwa Yanga ambao viungo wao hupendelea kucheza mipira mirefu kwenda kwa washambuliaji wa kati ama katika wings.
Kasi, umakini, na uwezo wa kutumia makosa ya timu pinzani katikati ya uwanja kwa wachezaji wa Yanga iliwasaidia katika mechi za ushindi wa 2-0, 2-0 dhidi ya mahasimu wao hao msimu uliopita. Nimeiona Simba jinsi inavyocheza msimu huu.
Wanategemea zaidi upande wa kushoto kupeleka mashambulizi mbele kutoka na uwepo wa Mohamed Hussein ambaye si mpotezaji wa mpira, mlinzi huyo wa kushoto amekuwa akitengeneza magoli ya Simba msimu huu baada ya kuondoka kwa Hassan Kessy ambaye alikuwa akifanya kazi hiyo msimu uliopita.
Kitendo cha Vicent kuendelea kucheza mbali ya goli lake kitawapa ushindi mwepesi Yanga ambayo washambuliaji wao, Donald Ngoma na Amis Tambwe hawana masihara hata kidogo.
Uwezo wa kupiga mashuti ya mbali yenye mwelekeo sahihi golini wa Thaban Kamusoko na Haruna Niyonzima unaweza kuwasaidia sana Yanga hasa ikiwa, Jonas Mkude, Mwinyi Kazimoto na Said Ndemla wataendelea kupoteza mpira hovyo katikati ya uwanja.
Deus Kaseke atakuwa tatizo kubwa kwa mlinzi ‘mzito’ Javier Bokungu ambaye hana kasi, pia si mwepesi. Ikiwa, Kaseke atacheza katika kiwango chake cha kawaida au zaidi ni yeye atakayeivuruga safu yote ya ulinzi ya Simba ambayo ukiachana na M-congoman huyo (Bokungu), pia yupo Mzimbabwe, Method Mwanjali ambaye pia hana kasi.
Kupitia kulia mwa uwanja upande wa Simba itafanya mlinzi mmoja wa kati wa Simba kutoa msaada mara kwa mara na jambo hilo litafungua nafasi za wazi zaidi katika beki ya kati na hilo likitokea Yanga watapata magoli ya kutosha.
Ili washinde mechi ya tatu mfululizo katika ‘ Dar-Pacha’ Yanga watapaswa kucheza kwa umakini katika safu yao ya ulinzi na kuongeza kasi katika sehemu ya kiungo kwa sababu wachezaji wa Simba hawakimbii na pasi zao hazina kasi.
Hilo litawasaidia kuipata mipira mingi na pasi zao ndefu katika maeneo ya wings zitawasaidia kufika haraka katika katika eneo la hatari la Simba.
Yanga wataifunga kirahisi Simba endapo watacheza kwa kasi na kuhakikisha kila shambulizi lao linakwenda katika mwendo wa kasi kwa maana Simba ni wazito kuanzia kwa golikipa hadi kwa walinzi wao.