SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumatano, 28 Septemba 2016

T media news

Manchester United ndio imemfanya Rooney awe hivi

Na Ayoub Hinjo

Rudi miaka kadhaa nyuma kisha kumbuka jinsi nahodha wa Manchester United Wayne Rooney alivyokuwa anajitoa kwa kila kitu pale Old Trafford. Alikuwa muhimili wa timu hiyo,kila jambo alilofanya ilikuwa ni kuipigania Manchester United.

Wengi walimbatiza majina mengi sababu ya ufanisi wake wa kazi pia uwezo wake wa kucheza nafasi nyingi ulimfanya aonekane ni mchezaji aliyekamilika zaidi uwanjani sababu alikuwa anazuia na kushambulia pia alikuwa mzuri katika kutengeneza nafasi za magoli na hata kufunga.

Nyakati zimeenda sasa Rooney amebadilika sana. Amekuwa kero kwa watu walewale ambao walikuwa wanamshangilia. Hivi sasa anapigwa vita hata na vyombo vya habari vilivyokuwa vinampamba.

Unadhani Rooney mwenyewe anapenda kuwa hivi!? Ila Manchester United wanatakiwa kujua kuwa wao ndio chanzo cha nahodha huyo kuwa kwenye ubovu wake.

Maisha ya Rooney yalianza kubadilika tangu RvP alivyoingia kikosini hapo ndipo alipoanza kubadilishwa nafasi tofauti tofauti sababu sehemu ambayo aliyokuwa anacheza amepatikana mtu wa uhakika zaidi.

Miaka ya hivi karibuni ametumika sana kama kiungo (mkabaji na mshambuliaji) sasa kwanini asipoteze ubora wakati timu yake inaamini Wayne anauwezo kuziba maeneo mengi ndani ya uwanja!?

Kwa umri wa Rooney na jinsi alivyotumika hakutakiwa kuwa tegemezi tena ila United walihitaji kumlinda tu tofauti na anavyopewa majukumu makubwa sababu huyu si yule ambaye alikuwa anaweza fanya kila kitu pekee yake.

Mfano hai upo Barcelona. Angalia walivyorahisisha maisha ya Iniesta. Hapewi majukumu mazito kama zamani sababu walishatengeneza mazingira ambayo hayamuathiri tena.

Kilichomtokea Pirlo pale AC Milan ndio kinachomtokea Rooney. Pirlo alipewa majukumu mazito licha ya umri wake kuwa umekwenda mwishowe akaonekana hafai lakini Juventus waliwafundisha jinsi ya kumtumia Pirlo.

Rooney hana ubora kama zamani lakini bado kuna kitu anaweza kukifanya kwa usahihi kabisa anapokuwa uwanjani. Rooney ana uwezo wa kupiga pasi sahihi na zenye madhara hilo ndilo United walitakiwa kulilinda kwa kumjengea mazingira rafiki ili waweze kunufaika naye katika uzee wake pia.

Inaonekana ni utamaduni wa timu za England kushindwa kulea wachezaji wao. Angalia pale Chelsea wanavyolia Terry akikosekana,sasa kwa umri wa Terry bado anategemewa pale darajani. Vivyo hivyo Liverpool kwa Gerrard.

Rooney anaweza kuwa sehemu ya kikosi cha kwanza kama atajengewa mazingira bora ili na yeye atoe alichonacho. United wamemfanya Rooney awe hivi wanapaswa kuliangalia ili heshima yake isitiwe mchanga.