MTUNZI:ENEA FAIDY
....Eddy alisimama kwa muda huku akiyashangaa yote yanayoendelea. Alishindwa kuamini kama kinachoendelea pale kilikuwa na ukweli ndani yake. Alifuta macho yake na kutazama tena, safari hii macho yake yalitua moja kwa moja kwa Doreen aliyekuwa amepiga magoti mbele yake huku akilia kwa uchungu na majuto mengi.
"Nisamehe Eddy kwq kukufanyia ukatili huu. Nimekutesa sana wewe na familia yako... Nisamehe tafadhali" alisema Doreen huku akilia kwa uchungu hali iliyodhihirisha majuto aliyokuwa nayo moyoni mwake. Hata hivyo Eddy hakuweza kuzungumza chochote zaidi ya kumtazama Doreen kwa hasira huku machozi yakimtiririka machoni mwake.
Aliumanisha meno yake kwa hasira huku akitamani kuiondoa roho ya Doreen kwani mateso aliyompa maishani mwake ilikuwa ni vigumu kusahaulika. Mateso aliyokuwa nayo yalijaa fedheha na aibu isiyositirika. Machozi yalimshuka taratibu machoni mwake huku akimtazama Doreen.
"Naomba unisamehe Eddy ili adhabu ninayopata ipungue walau kidogo... Nateseka Eddy" Doreen alizidi kumsihi Eddy lakini maneno yake ilikuwa ni kama kujilisha upepo kwani Eddy hakuukubali msamaha wake.
Wanawake waliokuwepo eneo lile walijisikia aibu kwa kuona wanawake wenzao wapo uchi wa mnyama. Wakatoa khanga zao na kuwapa akina Doreen wazivae lakini hata hivyo ilikuwa vigumu kwa akina Doreen kupokea khanga zile kwani maumivu yalikuwa Makali mno kwenye miili yao. Kila Mara walihisi moto ukiwawakia katika ngozi zao. Ikawabidi wanawake wale wawafunike kwa lazima ili kuwasitiri.
Ghafla mwili wa Maimuna ukaanza kubadilika na kuwa mweusi kama mkaa. Akajiviringa viringa kama nyoka pale sakafuni huku akitoa mlio kama wa mbuzi kisha akatoweka mbele ya macho ya watu. Wote waliogopa sana, baadhi ya watu walijikaza kisabuni na kuendelea kubaki pale huku wengine wakikimbia sana na kuondoka eneo lile.
Doreen alibaki pale huku akiendelea kumsihi Eddy amsamehe. Lakini Eddy alikuwa na moyo mgumu sana wa kumsamehe kiumbe yule.
"Hustahili kuishi Doreen... Kufa tu.." Alisikika Eddy kwa sauti iliyojaa hasira.
"Kweli! Afe tu huyu! Tumuue!" Walisikika Raia waliokuwepo eneo lile.
"Nitakufa ndio ila naomba unisamehe.. Najua nimekukosea sana... Sitaki nife kabla hujanisamehe!" Alisema Doreen.
"Kwa mateso uliyonipa siwezi kukusamehe... Umenitesa sana... Sijui nani amekuadabisha namna hii na kukudhalilisha hivi... Amenifurahisha sana" alisema Eddy kwani hakujua lolote linaloendelea kuwa Dorice ndiye aliyefanya yote hayo.
"Na kwa jinsi ulivyonifanyia.. Daima siwezi kumwamini mwanamke! Naapa!" Alisema Eddy lakini kuna sauti ilimnong'oneza masikioni mwake
"Usiseme hivyo... Niamini Mimi" Eddy alishtuka sana akaangaza macho huku na kule pasipo kuona mtu aliyemnong'oneza. Sauti ile haikuwa ngeni sana masikioni mwake ila alishindwa kujua ilikuwa ya nani. Akatafakari kwa muda kisha akaipotezea sauti ile na kuendelea kumtazama Doreen.
"Eddy hutaki kunisamehe?" Aliuliza Doreen kwa sauti ya upole. Eddy akatafakari kidogo, akagundua kutomsamehe binadamu mwenzake ni kosa kubwa kwani yeye hutenda dhambi nyingi lakini husamehewa na Mungu.
"Nimekusamehe.. Ila sitokusahau!"
"Asante..."