SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumatatu, 5 Septemba 2016

T media news

BARCELONA WAMEGEUZA UPANDE WA PILI WA WEMBE


Na Athumani Adam

Kutoka kwenye maisha ya  kimaskini kule Port Alegre hadi utajiri wa Avenue Park jijini New York. Kazi ya miguu yake ilimpeleka  barani Ulaya. Aliishi  Paris akaenda Barcelona na baadae Milan. Kwa sasa ni tajiri anaweza kufanya chochote kupitia fedha alizovuna kwenye vilabu vya Paris Saint German, Barcelona na AC Milan

Sehemu ya utajiri wake ulitokana na matangazo ya biashara. Alikuwa balozi wa kampuni ya vifaa vya michezo Nike pia alitangaza na kampuni ya vinywaji baridi Pepsi.

Ukiondoa utajiri pia ni mmoja ya watu maarufu duniani. Alikubali kuacha kutumia jina lake la Ronaldo ili kujitofautisha na Ronaldo De Lima. Alidhani asingepata umaarufu kama kungekuwa na Ronaldo wawili kwenye kikosi cha Brazil kwenye kombe la dunia 2002 kule Korea Kusini na Japan.

Akaamua kujiita Ronaldinho Gaucho,  mchezaji bora wa dunia mwaka 2004 na 2005. Barcelona wameamua kumrudisha kwa mara nyingine. Ronaldinho amepewa kazi ya kuwa balozi wa klabu yake ya FC Barcelona kule jijini New York. Gaucho atakuwa na kazi ya kuitangaza Barcelona lengo likiwa ni kujiongezea idadi ya mashabiki.

Barcelona ni kama wamegeuza sarafu tu, baada ya kufaidika na Gaucho ndani ya uwanja kwa miaka minane sasa wanafaidika tena nje ya uwanja.

Barca ni klabu ya wanachama, haijakodiwa wala hajapewa tajiri mmoja. Msingi wa maendeleo yake ni kuwa na mashabiki wengi duniani. Wamemrudisha Gaucho kundini lengo ni kuwasaidia kuitangaza Barca kule America ya Kaskazini.

Vilabu pamoja na ligi kubwa duniani wamegundua moja ya njia ya kujitangaza ni kupitia legends. Hawa ni watu wanaopendwa duniani, tupo tayari kujaza uwanja wa taifa kwenda kuangalia mechi ya Barcelona au Madrid Legends sababu tunawapenda kina Fernando Redondo.

Jezi ya Barcelona imesambaa duniani kote sababu ya soka safi bila kusahau kazi  inayofanywa na mabalozi. Leo hii hawa Legends wa Barca hawaji kucheza Dar au Kampala halafu wakaondoka bure. Mashabiki ndio msingi wa maendeleo, ndio maana wanatumiwa kina Gaucho sababu ni maarufu.

Kina Gaucho wana wafuasi pande nne za dunia. Wanapendwa na wafuasi wao, wapo tayari kuvaa kile wanachovaa pia watanunua kile watachotangaza. Vilabu, ligi kubwa duniani na makampuni ya biashara wapo tayari kuwamwagia fedha kina Gaucho ili watangaze bidhaa zao.

Kwa kujua thamani ya Legends, kwenye klabu ya Madrid kuna aina moja ya uwanachama unaitwa Ambassodor Membership. Hawa ni wanachama mabalozi ambao kazi yao kubwa ni kuitangaza Madrid duniani kote.  Hawa ndio wale kina Luis Figo ambao walikuja Tanzania kucheza  legends wa bongo.

Hawa Ambassador Membership hawalipi ile euro 145 ambayo ni ada ya uanachama kwenye klabu ya Madrid. Wanaingizia klabu zaidi ya pesa hiyo kupitia ushawishi wao duniani kote.

Wachina walimchukua David Beckham kama Balozi ili awatangazie ligi yao vilevile kuhamasisha vijana wa kichina kuupenda na kucheza mchezo wa mpira wa miguu. Legends ni kama viwembe, upande wa kwanza wa makali yao walikuwa wakati wanacheza. Ufundi wao uwanjani ulileta faida ya mataji kwa vilabu pamoja na mataifa.

Sasa wanatumia upande wa pili wa makali yao kuleta mafanikio ya vilabu nje ya uwanja. Barcelona wamemchagua upande wa pili wa Gaucho kuvuna wachotaka kutoka kwenye taifa ambalo mpira wa miguu sio mchezo namba moja.