SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumatatu, 5 Septemba 2016

T media news

Raia, watalii Arusha kulindwa kwa CCTV

MKUU wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo, amesema anakusudia kuimarisha usalama wa mkoa huu kwa kufunga kamera za CCTV zitakazosaidia kubaini matukio ya uhalifu na wahalifu.

Alisema tayari mkoa huu umeanza mchakato wa kutekeleza mpango huo. Gambo alisema hayo mwishoni mwa wiki alipotembelewa na Balozi wa Sweden nchini, Katarina Rangnite , akiwa na ujumbe wake wa wabunge kutoka nchini humo.

"Tunakusudia kuongeza usalama mkoani mwetu kwa kufunga kamera za CCTV zitakazotuonesha matukio ya uhalifu na wahalifu watakaokuwa wakiwasumbua wananchi wa Arusha, watalii na hata wawekezaji wa mkoani mwetu,"alisema.

Alisema mkoa umeshaonesha nia ya kuhakikisha unakuwa salama wakati wote na uko tayari kuwekeza katika mfumo huo, ili kuwaongezea ulinzi wananchi na mali zao, watalii na wawekezaji.

"Tunapokuwa na uhakika wa kudhibiti wahalifu tunakuwa na uhakika wa usalama na kuwavutia watalii na wawekezaji. Pia wananchi wanakuwa na amani,"Gambo alisema.

Katika hatua nyingine, alimuomba Balozi wa Sweden ashirikiane na mkoa huu katika kampeni ya kulinda vyanzo vya maji, ili kuwezesha mradi mkubwa wa maji unaosimamiwa na Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka (Auwasa), utekelezwe kwa mafanikio.

Gambo alisema kuwa Jiji la Arusha limepewa zaidi ya Sh bil 476 ili kumaliza tatizo la maji.

Kwa upande wake, Balozi Rangnite alikubali kuwekeza katika mfumo huo wa CCTV unaotegemewa kufanya kazi kwa saa 24 kila siku, kwa sababu ndio wenye usalama zaidi.

Aidha, alisema kuwa Sweden ina wataalamu waliobobea katika mifumo hiyo ya usalama wa miji hivyo kumuomba Gambo awasilishe ombi lake kwa maandishi mradi huo utekelezwe.