Wastani wa Sh milioni mbili zinatumika kumtibu majeruhi mmoja wa pikipiki, jambo ambalo limezifanya hospitali zinazowapokea majeruhi hao, kuzidiwa na gharama hizo za matibabu.
Madaktari kutoka Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) wamesema kwamba kwa sasa kila siku, wanapokea wastani wa majeruhi kati ya 50 na 60, jambo ambalo linaiwia vigumu taasisi hiyo kutoa huduma za uhakika kwa majeruhi hao.
Gharama hizo zinatokana na vyuma vinavyotumika kuwatibu majeruhi wa mifupa mirefu kuagizwa nje ya nchi, jambo ambalo linaelezwa na madaktari kwamba kutokana na idadi ya majeruhi kuongezeka kila siku, inailazimu MOI kukabiliwa na upungufu wa vifaa hivyo.Kutokana na kuongezeka kwa majeruhi hao wa bodaboda, Jumuiya ya Madaktari Wakristo (TCMA) wametumia mkutano wao wa mwaka uliomalizika juzi, kujadili jambo hilo na kueleza kuwa ajali zinazotokana na bodaboda ni janga la taifa kutokana na kuziongezea gharama za upasuaji hospitali.
Kwa hali hiyo, wameziomba mamlaka za masuala ya usalama barabarani, kuhakikisha zinatunga sheria kali zitakazowabana wapanda na waendesha bodaboda ili kuepusha taifa kuwa na walemavu wengi wa ajali za vyombo hivyo vya usafiri.