SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumamosi, 27 Agosti 2016

T media news

Tanzania kuwa na wataalamu 500 wa gesi na mafuta

WAZIRI wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo amesema baada ya miaka 10 ijayo, Tanzania itakuwa nchi ya kwanza Afrika Mashariki kuwa na wataalamu wa gesi na mafuta kwa kuwa na wataalamu Watanzania 500.

Alisema wamejiwekea malengo hayo na yanakaribia kukamilika, kwa kuwa na Watanzania wenye elimu ya gesi na mafuta kuanzia ngazi ya Stashahada, Shahada, Shahada ya Uzamili na Uzamivu kutoka vyuo vya ndani na nje ya nchi.

Muhongo aliyasema hayo jana wakati akiwapa vyeti vya ufadhili wa Serikali ya China wanafunzi 20 wa Kitanzania, wanaoenda kusoma masomo ya uzamili na uzamivu kwa miaka mitatu nchini China.

Alisema serikali imeweka lengo la kuwa na wataalamu wa sekta ya gesi na mafuta 500, jambo litakalofanya iwe nchi yenye wataalamu wengi wa sekta hiyo katika nchi za Afrika Mashariki.

Alisema wataalamu hao, watapatikana kupitia Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Chuo cha Madini Dodoma na wanafunzi wanaopelekwa nje ya nchi kwa mafunzo katika nchi za China Norway na Uingereza kwa ufadhili wa wizara na nchi husika.

“Nchi ya China imekuwa ikifadhili wanafunzi 25 kwa miaka mitano na mpaka sasa tayari wanafunzi 62 wamepatiwa elimu hiyo huku wizara ikifadhili wengine katika nchi, kwa sasa bado wataalamu waliopo hawatoshi katika sekta za umma hata sekta binafsi,” alisema.

Profesa Muhongo aliwataka wanafunzi hao 20, kuhakikisha wanaenda kusoma na siyo kufanya kazi za kubeba nguo, kwani siyo lengo la ufadhili huo na itakuwa aibu kwa nchi.

Akizungumzia upatikanaji wa wanafunzi kupata ufadhili huo, Profesa Muhongo alisema walitangaza na walijitokeza 89 walioomba na kuchambuliwa na watendaji wizarani, lakini baadaye Waziri mwenyewe alifanya uchambuzi na kuwaondoa wanane, alioona hawakuwa na sifa za kusoma.

“Hawa waliopo wamechaguliwa kwa haki kwani kabla ya kupelekwa ubalozini, mimi mwenyewe nilipitia majina hayo na kuhakiki baadaye tulitofautiana na watendaji wangu, nikakata majina manane, hapa lazima haki itendeke hata kama mwanangu, nitamwambia hapa huwezi,” alisema Muhongo.

Naibu Balozi wa China nchini, Gou Haodong aliwasihi wanafunzi hao kuwa mabalozi wazuri wa Tanzania nchini China, kwa kufuata mila na desturi za nchi hiyo huku wakihakikisha wanafanya kile kilichowapeleka.