Na Athumani Adam
Claudio Bravo amekuwa mchezaji wa nane kusajiliwa na kocha Pep Guardiola ndani ya klabu ya Manchester City. Uhamisho wa golikipa huyo raia wa Chile kutoka klabu ya FC Barcelona ni ishara kwamba ule ufalme wa kipa namba moja wa City Joe Hart umefika ukingoni pale Etihad.
Japokuwa uwezo wa Bravo kuanzisha mashambulizi kutokea nyuma ndio sababu iliyomvutia Guardiola kufanya usajili huu, makala hii inakupa sababu tatu ambazo zimechangia Bravo kuondoka Fc Barcelona baada ya uchunguzi kutoka kwenye vyanzo vya kuaminika duniani
MSHAHARA MDOGO UWEZO MKUBWA
Kwenye dirisha hili la usajili Barcelona walikuwa na mpango wa kumuongezea Claudio Bravo mkataba kabla ya ule wa awali ambao ulitarajiwa kumaliza mwaka 2018. Bravo alitegemea mkataba wa kuanzia miaka miwili pia kuongezewa mshahara wa mwishoni mwa wiki.
Barcelona walishindwa kufikia matarajio ya Bravo pale walipoleta mkataba wa mwaka mmoja pamoja na mshahara ambao haukufika kiwango alichokita Bravo. Hadi anaondoka kwenye klabu ya Barcelona Bravo alikuwa anapokea mshahara wa Euro 33,500 kwa wiki huku golikipa namba mbili Marc Andre Stegen analipwa Euro 55,000 kwa wiki.
BIFU NA MARC ANDRE TER STEGEN
Kauli za Kipa Marc Andre Ter Stegen dhidi ya Bravo zimechangia kuleta bifu la chinichini baina yao. Mara kwa mara Ter Stegen amekuwa akitoa kauli kuwa anataka apewe nafasi ya kucheza hususani kwenye La Liga la sivyo ataihama klabu hiyo zimekuwa hazimvutii Claudio Bravo.
Kocha wa Barcelona Luis Enrique amekuwa akimpa nafasi zaidi ya kucheza Claudio Bravo ukilinganisha na Mjerumani Ter Stegen.
USHAWISHI WA FAMILIA
Bravo na mkewe Carla Pardo walikuwa na mipango ya kuhamia England. Hata watoto wao kule nchini Spain kwenye jiji la San Sebastian wanasoma shule zinazofundisha kwa lugha ya kiingereza. Hivyo uhamisho huu kwa Bravo hautakuwa na athari yeyote kwenye familia yake