RAIS mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete ametaja mambo muhimu aliyoyapigania kwa nguvu zake wakati wa kipindi chake cha miaka 10 ya urais.
Akizungumza mjini Bagamoyo wakati wa sherehe ya kumkaribisha nyumbani baada ya kukabidhi uenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa Mwenyekiti mpya Rais John Magufuli, Kikwete alisema alipigana kufa kupona kukabili mambo hayo ili asiwaangushe wana Bagamoyo anakotoka na Mkoa wa Pwani kwa ujumla.
Akibainisha jambo la kwanza, Kikwete alisema lilikuwa ni jambo la kutokubali kushindwa na kwamba dhana ya kutokubali kushindwa jambo ilikuwa ikimweka katika wakati mgumu kutokana na ukweli kwamba kushindwa kwake kungekuwa ni kushindwa kwa watu wa Bagamoyo.
“Kila nilipokuwa nikifikiria kushindwa kwenye jambo lolote la uongozi wangu kwa nchi au kwenye chama nilikuwa napata wakati mgumu sana. Namshukuru Mungu kwani nilifanikiwa kwa mambo mengi.”
Alitaja mambo ambayo anadhani aliyafanya vizuri kutokana na kutokubali kushindwa kuwa ni pamoja na suala la utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Alisema hata hivyo katika utekelezaji huo wa miradi, iliibuka changamoto ya pili iliyomweka katika mazingira magumu ya kupambana ili kupeleka maendeleo katika eneo alilotoka huku akisema: “Katika kupeleka maendeleo huwezi ukapendelea sehemu uliyotoka au, pia suala la kuwanyima maendeleo ni kitu ambacho hakiwezekani.”
Alisema suala hilo liliibua dhana kwamba anaipendelea Bagamoyo akibainisha kuwa kauli hizo zilikuwa zikitolewa hadi na watu wenye kuaminika, wakiwemo wabunge akitoa mfano kuwa walidai amehamisha fedha za ujenzi wa barabara kutoka eneo lingine na kuzihamishia kwenye ujenzi wa barabara ya Msata Bagamoyo.
“Hali kama hii ilikuwa inanipa wakati mgumu kwani kila sehemu inataka maendeleo na nisingeweza kutofanya maendeleo kwa watu wa Bagamoyo kwani hata wao wanahitaji maendeleo kama sehemu nyingine,” alisema Kikwete.
Alisema jambo la ajabu ni kwamba dhana hiyo ilikuwa tofauti kwani ilikuwa kinyume chake, kwa vile kuna wakati ilibidi ahamishe fedha kutoka Bagamoyo na kufanya ujenzi kwenye maeneo ya Geita, Sengerema hadi Usagara wakati huo Waziri wa Ujenzi akiwa Basil Mramba.
“Hili hawakuliona, wao waliona la mimi kuhamishia fedha Bagamoyo. Namshukuru Mungu kwani ujenzi wa barabara katika maeneo yote ulikwenda vizuri. Katika uongozi wangu tulifanya kazi ya kuleta maendeleo makubwa na tumeiacha nchi mahali pazuri.”
Jambo la tatu, alisema lilikuwa ni mikikimikiki iliyosababishwa na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, na kwamba uchaguzi huo ni miongoni mwa mambo yaliyomuweka katika wakati mgumu.
Alisema hata hivyo anamshukuru Mungu kwa uchaguzi huo kumalizika salama.
“Hili nalo lilikuwa gumu sana kwangu lakini nalo lilipita kwani watu walishindana lakini hawakupigana wala kumwaga damu na uchaguzi ulipokwisha maisha yaliendelea salama kabisa,” alisema Kikwete.
Rais mstaafu Kikwete alitaja jambo la nne; madai kuwa alikuwa na mpango wa kubadili Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili aendelee kubakia madarakani.
“Hapa napo kulikuwa na mtihani wa aina yake maana wapo ambao walisema nina mpango wa kubadili Katiba lakini wapo waliosema Rais gani hata hafanyi mpango wa kubadili Katiba ili aendelee kukaa madarakani, “ alisema.
Katika mkutano huo Rais mstaafu Kikwete, alisema Watanzania wanapaswa kumuombea Rais John Magufuli ili aweze kuleta maendeleo kwani ni mpenda maendeleo hivyo lazima asaidiwe aweze kuleta maendeleo ya watu.
Akizungumza kuhusu CCM, alisema chama hicho kiko vizuri na kwamba hakuna chama inachoiweza CCM kwa vile ni imara na kina viongozi madhubuti.
Katika sherehe hiyo ambayo ilihudhuriwa na familia ya Kikwete, rais huyo mstaafu alipewa zawadi mbalimbali, ikiwa ni pamoja na mifugo kama vile ng’ombe, mbuzi, kuku, bata, mavazi ya jadi na vitu mbalimbali ambavyo vilitolewa na wananchi wa Mkoa wa Pwani.