SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Ijumaa, 3 Juni 2016

T media news

YANGA WANA MBWEMBWE,YANGA SIYO TIMU YA KAWAIDA

Na Richard Leonce
Katika taifa letu hili pendwa la Tanzania kuna vitu vipo kama vilivyo. Ni ngumu kuvibadili kwa sababu ni lazima uanze kubadili kwanza mioyo ya watu, kitu ambacho si cha kawaida, japo mara nyingine huwa tuna nia ya kubadilika. Kuna siku niliwahinkusikiabkauli kutoka kwa kiongozi mmoja mwenye mamlaka akisema kuanzia Januari 1, 2016 itakua ni marufuku abiria kusimama kwenye daladala. Nilijua haitokua, na haikua.

Kauli hiyo kwangu haikutofautiana na kauli ya kamati ya uchaguzi ya TFF kwamba itasimamia uchaguzi wa klabu ya Yanga. Tena nilishtuka niliposikia hayo ni maagizo ya Serikali kupitia Baraza La Michezo (BMT) Hapo ndipo nilipomkumbuka aliyekua kocha wa Azam FC, Stewart John Hall alipogundua kwamba timu yake itakutana na Yanga kwenye fainali ya kombe la ASFC. Alitoa kauli zake kwa lugha yake bila kupindisha maneno masikini mzee wa watu.

Alisema hakupenda Azam ikutane na Yanga kwa sababu Yanga ni timu hatari sana. Ukiacha kua na kikosi bora uwanjani chenye uwezo wa kushindana, lakini Yanga ina mashabiki wengi sana ambao wengine ndiyo viongozi wa soka, na wengine ndiyo waamuzi. Stewart alitoa ukweli wake ambao najua hakuumaliza. Bila shaka ukiweza kupata nafasi ya kuketi nae anaweza kukuambia uwezo usio wa kawaida wa Yanga.

Kwa jinsi ninavyoijua Yanga nilijua Maneno ya Aloyce Komba kutoka kamati ya uchaguzi ya TFF hayatotofautiana na maneno ya yule kiongozi aliyesema itakua marufuku kwa daladala kusimamisha abiria ifikapo Januari 1 iwapo wenye Yanga yao hawatopendezwa na hilo. Tusome basi mpaka la saba walau ili hata yale yanayotendeka kwa Kiswahili tuweze kuelekezana kwa urahisi. Hivi timu inaposigina katiba yake labda kwa kutofanya uchaguzi, tena kwa makusudi, kwa kipindi kirefu tu, unapaswa kuifanya nini?

Tena tukumbuke kwamba kinachotokea Yanga leo kuna siku kitatokea Tukuyu Stars, kuna siku kitatokea Ashanti, Simba, Mbao FC nk. Je wao pia watafanyiwa hiki inachotaka kufanyiwa Yanga leo? Kimsingi, Yanga wamevunja katiba yao, kwa kufanya hivyo tayari wamevunja katiba ya TFF na ya FIFA pia. Na mimi naamini BMT na TFF hawakupaswa kusimamia uchaguzi wa Yanga, bali walipaswa kuishusha daraja, au kuifuta kabisa. Lakini ni nani mwenye ubavu huo?
Unadhani Yanga ni timu ya kawaida? Wote tunaijua Yanga inapotaka jambo lake. Yanga wanapotaka uchaguzi huwa wanaufanya hata kama muda wake haujafika. Muulize mtu mmoja anaitwa Loyd Nchunga atakuambia.Yanga siyo ya kawaida, ina wenyewe. Na hao wenyewe wakilitaka jambo lao hata kama ni wangapi hawataki, huwa linapata baraka na kuhalalishwa.

Unaweza kushangaa Yanga kukataa logo ya mdhamini wa ligi isikae kwenye jezi yao mpaka ibadilishwe rangi, Kabla hujakaa sawa ukasikia Yanga hawataki kukabidhiwa kombe wakiwa Mtwara, wanataka mchezo wao wa ugenini uhamie Dar es Salaam. Hayo yote hiwa yanafanyika kwa sababu Yanga siyo timu ya kawaida.

Sasa pamoja na TFF kuamua kutangaza uchaguzi wa Yanga, kitendo ambacho kilikua ni kwa faida yao ingawa siyo sahihi lakini Yanga bado hawataki uchaguzi wao usimamiwe na TFF. Na wana haki, kwa sababu siamini kama TFF inawajua wanachama wenye sifa za kuchagua na kuchaguliwa pale Yanga.

Yanga wameamua kutangaza uchaguzi wao ghafla tu. Tena wanataka kuufanya June 11 lakini ajabu ni kwamba mpaka naenda kabatini kuchukua kalamu yangu walikua bado hawajatangaza kamati yao ya uchaguzi. Ni ajabu na kweli, Hii ni Yanga ile ile. Yanga yenye mbwembwe za hali ya juu sana. wanataka uchaguzi wao ingawa ukweli ni kwamba pale Yanga hakuna uongozi halali kikatiba.

Lakini mimi naamini wataufanya, Wataanza kutoa fomu zao, na utaona wale wagombea wao uliowatarajia wakichangamkia fomu. Wale wazito wenye Yanga yao, achana na wale wawili watatu walioenda kuzichukua TFF.

Wakishazichukua, watafanya kampeni zao kwa muda huo huo mfupi, kisha watamchagua yule ambae uongozi wao hewa uliopo hivi sasa unamtaka, kisha wataendelea na maisha yao. Wakati huo TFF na kamati zake watakua bado wanaendelea na vikao ambavyo siamini kama vitakua na jipya.

Hii ndiyo Yanga. Na hapa Yanga wameamua jambo lao. Wanamtaka mwenyekiti wao.
Kuna siku wenye Yanga yao walikua hawamtaki mwenyekiti wao, wakaamua timu ifungwe ili ajiuzuru wafanye uchaguzi.
Lakini sasa wanamtaka Mwenyekiti wao na si Uchaguzi, katiba ilitaka uchaguzi na wao hawakuutaka, sasa wameamua kuufanya ndani ya siku 10 na hawataki wafanyiwe na mtu.

Kweli Yanga siyo timu ya kawaida.