SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Ijumaa, 3 Juni 2016

T media news

KARIBU XHAKA, MGENI MWENYE SODA YAKE.


Na Richard Leonce
Siku moja nilienda kumtembelea rafiki yangu mmoja nyumbani kwake. Nikiwa njiani nikanunua soda ya kopo nikaweka kwenye begi langu, nilipofika kwa rafiki yangu nikakuta ameniwekea soda mezani. Nikacheka sana kisha nikamwambia mimi nina soda yangu.

Hiki kisa hakitofautiani sana na usajili wa huyu kijana mwenye umri wa miaka 23 aliyesajiliwa akitokea Borussia Monchengladbach. Umesikia sentensi zake?

>>>Mimi ni mchezaji imara, Arsenal imeongeza mtu mwingine anayejua mapambano.

Anaongeza kwamba anafurahi kujiunga na ligi ya England kwa sababu kule Ujerumani alikotoka pamoja na kwamba kuna soka la mabavu lakini waamuzi wa kule ni wakali kwa hilo, tofauti na waamuzi wa England ambako ubabe siyo hiyari.

Huyu si mwingine, ni Mswiss Granit Xhaka, Mshika bunduki mpya ambaye amegharimu Pounds ambazo hatujawekewa wazi japo ni kuanzia £25M ambazo zinaweza kuongezeka hadi £35M kulingana na kwango na msaada wake kwa timu utakavyokua.

Xhaka hatanii anaposema yeye ni mchezaji imara. Hapa unamzungumzia mtu ambaye alicheza mechi 9 za msimu wa 2014/15 akiwa amevunjika mbavu, na anakuambia maumivu alikua anayapata usiku tu akiwa amejipumzisha, lakini alipokua kiwanjani alikua akiwaza ushindi tu.

Siyo mtu wa kawaida sana huyu, ni mtu mwenye rekodi ya kukusanya kadi nyingi nyekundu katika umri mdogo tangu ligi ya Bundesliga ianzishwe. Amekutana na kadi hiyo mara 5
, na ana umri sa miaka 23 pekee. Kadi 3 kati ya hizo amezipata msimu uliopita.

Hii siyo sifa nzuri ya kuja nayo katika ligi ya EPL iliyosheheni timu pendwa kama Man UTD na Liverpool. Rafiki yangu Nicasius Agwanda huwa anawashauri wachezaji kama hawa kuvua viatu vyao kabla hawajalikanyaga zuria la EPL kwa sababu waamuzi wa EPL wakati mwingine huzidisha makosa ya kibinadamu wanapochezesha michezo ya timu pendwa.

Sababu za usajili wa Xhaka si ngumu, ni kuondoka kwa viungo Mikel Arteta, Thomas Rosicky na Mathieu Flamini kwa mpigo. ni lazima upate watu wa kuziba hizo nafasi.

Lakini unalitazama ongezeko la huyu mtu mahali ambapo kuna Francis Cocquelin, Mohamed Elneny, Santi Cozorla, Jack Wilshere na Aaron Ramsey. unajiuliza huyu mtu anakuja kuleta nini?

Unatazama ada yake ya uhamisho unagundua ni mchezaji anaekuja kushika nafasi ya 3 kwenye orodha ya wachezaji ghali zaidi wa muda wote wa Arsenal nyuma ya Mesut Özil na Alexis Sanchez. moja kwa moja huyu ni mgeni anaekuja na soda yake huyu. Hahitaji kununuliwa nyingine.

Yaani siyo ile aina ya wachezaji wanaosajiliwa kisha wakapewa nafasi ya kuizoiea ligi, huyu yupo kamili na anaingia kikosini moja kwa moja. Ligi ya Uingereza ni ngumu sana, inahitaji watu wenye uzoefu wa mikiki mikiki na ikibidi wakorofi. Viungo wenye uwezo mkubwa wa kufanya ‘Tackling’ na kushambulia bila kuchoka. Na hii ndiyo sifa kuu ya Granit Xhaka

Xhaka anafurahi zaidi akicheza kama kiungo wa chini, lakini ana faida kubwa kwa sababu ana uwezo mkubwa sana wa kupiga pasi, hii ni tofauti kidogo na Francis Cocquelin ambaye anahitaji msaada wa haraka anapokua na mpira. Xhaka ana uwezo wa kutackle kwenye eneo lake kisha akauhamishia mpira katika eneo la kushambulia ndani ya sekunde 10, lakini ana uwezo wa kufunga pia, amefunga mabao 12 katika Bundesliga na 6 katika timu yake ya taifa ya Uswiss.

Arsene Wenger aliwahi kumbadili Mikel Arteta kutoka eneo la kiungo wa kushambualia, kuwa kiungo wa kukaba katika harakati za kupata ubora wa mtu kama Xhaka, Arteta alifanikiwa kiasi lakini hakutoa kile hasa ambacho ligi ya Uingereza inahitaji. Viungo wa aina ya Xhaka ni wachache sana, ni aina ya watu kama Xabi Alonso. Dunia inawapata wakiwa kwenye vifurushi tofauti tofauti na ndiyo maana Xabi amedumu kwa muda sasa kwenye soka kwa sababu watu wa aina yake si wengi.

Sasa anakuja kukata kichwa cha nani ndani ya kikosi?
Hii hainipi shaka kabisa kwa sababu kwa aina ya uchezaji wa Cocquelin, si salama kuwa nae kwa dakika 90. Cocquelin anaweza kukutana na kadi ya njano katika dakika ya 14 tu ya mchezo pale Old Traford nyumbani kwa Manchester United. Kama una Xhaka kwenye bench au kinyume chake inapunguza presha.

Lakini uwepo wake pia unaongeza machaguo katika eneo la kiungo. Tumeshuhudia majeraha yakitugharimu kwa kiasi kikubwa na kwa miaka mingi tumekua tukimtaka Arsene Wenger asajili kiungo mkabaji. Kwa aina ya uchezaji wa Xhaka, kwa roho yake mbaya, kwa kipaji chake cha uongozi na ukorofi wake, sitoshangaa si tu akipata nafasi ya kudumu mapema kikosini, bali hata akija kurithi kitambaa cha unahodha siku moja.

Huu ni wakati ambao Aaron Ramsey anapaswa kutambua kwamba siku za Arsene Wenger zinahesabika. Anapaswa kuimezea mate nafasi ya Santi Cazorla ambaye umri unaanza kuipunguza kasi yake huku akitambua kwamba Mohamed Elneny tayari amejipambanua kama mtu anaestahili kuvaa viatu hivyo.

Ni wakati ambao Jack Wilshere anapaswa kukemea majeraha yake kwa sababu Mimi nitaipenda zaidi pacha ya Xhaka na Wilshere. Lakini Wilshere pamoja na kwamba alikulia hapa,bado tulimpeleka hotelini kabisa Bolton tukamnunulia soda, sasa huyu Xhaka yeye anaonekana amekuja na soda yake.
Tukutane juma lijalo.