Jeshi la Polisi nchini limetoa wito kwa wamiliki wa silahi kujitokeza na kuhakiki silaha zao katika Wilaya wanazoishi kabla ya kumalizika kwa zoezi hilo mnamo Juni 30 mwaka huu.
Hayo yalisemwa na Msemaji wa Jeshi hilo Kamishna Msaidizi Advera Bulimba alipokuwa akiongea na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam.
“Serikali imetoa muda wa miezi mitatu kukamilisha zoezi hili muhimu na tayari miezi miwili imepita hivyo wale ambao bado hawajahakiki silaha zao kuzikakiki sasa kabla ya Juni 30 ili kuepukana na usumbufu” alisema Kamshna Msaidizi Bulimba na kuongeza kuwa:
“Natoa wito kwa watu wote wanaomiliki silaha kinyume na sheria kusalimisha silaha hizo katika vituo vya polisi, ofisi za serikali na kwenye nyumba za ibada na watakaofanya hivyo ndani ya muda ulipangwa hawatachukuliwa hatua zozote za kisheria”.
Aliongeza kuwa baada ya muda ulipangwa na Serikali kupita na wamiliki hawajahakiki silaha zao Jeshi la Polisi nchini litaendesha operesheni kali kuwakamata wale ambao hawakujitokeza katika zoezi la uhakiki na hatua kali zitachukuliwa ikiwemo kufutiwa leseni na silaha zao kutaifishwa na kuwa mali ya Serikali.
Aliwaomba ndugu wa wale walikuwa wakimiliki silaha ambao wamefariki au ni wagonjwa wasalimishe silaha hizo katika vituo vya Polisi kwa niaba ya ndugu zao ndani ya kipindi cha uhakiki wa silaha.
Zoezi la uhakiki wa silaha lilianza Machi 21 mwaka huu kufuatana na sheria ya usimamizi wa silaha na risasi ya mwaka 2015, ambapo kifungu cha 66 cha sheria hiyo kinamtaka kila mmiliki kuhakiki kumbukumbu za silaha yake au risasi pale anapoamriwa na mamlaka.
Lengo la kuhakiki kumbukumbu za wamiliki wa silaha ni kupata taarifa sahihi za wamiliki hao zitakazosaidia kubaini wale wote wanaomiliki kinyume na sheria, kuwafahamu wamiliki waliohama na kuhamia makazi mapya, kuwafahamu wamiliki waliofariki ili kuzuia vitendo vya uhalifu na uvunjwaji wa amani nchini.